Goma: Mamia ya watu wakamatwa na M23 katika uvamizi uliozua utata
(last modified Thu, 15 May 2025 03:10:07 GMT )
May 15, 2025 03:10 UTC
  • Goma: Mamia ya watu wakamatwa na M23 katika uvamizi uliozua utata

Vuguvugu la AFC/M23 Katika mji wa Goma na vitongoji vyake, limekuwa likifanya uvamizi na na kuwakamata kwa siku kadhaa likidai kuwa watu hao wanahusika na mauaji, uporaji na utekaji nyara.

Wasiounga mkono kundi la M23 wanasema kuwa linawateka nyara na kujaribu kuwaajiri vijana kwa nguvu katika safu zake.

Mwishoni mwa juma meya wa jiji la Goma Julien Katembo aliwaambia waandishi wa habari kuwa watu waliowakamata ni pamoja na "Askari wa FARDC, FDLR, Wazalendo na wahalifu wengine".

Msako wa kuwasaka na kuwakamata washukiwa uliendelea siku ya Jumatatu na Jumanne, hasa katika maeneo ya kaskazini mwa mji wa Goma, ambako vitendo vya mauaji, uporaji na utekaji nyara vimeripotiwa kwa muda.

Katika wiki chache zilizopita, zaidi ya mauaji 10 yameripotiwa katika jiji la Goma.

Kundi la M23, lililo katikati ya mzozo wa mashariki mwa Kongo, limeongeza mashambulizi yake tangu Desemba, likiteka miji muhimu ikiwemo Goma na Bukavu.

Kinshasa na wengine wanailaumu Rwanda jirani kwa kuwaunga mkono M23 — madai ambayo Kigali inakanusha.

Mwezi Machi, Rais wa Kongo Felix Tshisekedi na Rais wa Rwanda Paul Kagame walikubaliana usitishaji mapigano katika mazungumzo yaliyosimamiwa na Emir wa Qatar huko Doha. Licha ya makubaliano hayo, mapigano yameendelea katika maeneo ya jimbo la Kivu Kaskazini.

Mwezi Aprili, Waziri wa Mambo ya Nje wa Kongo Therese Kayikwamba Wagner na mwenzake wa Rwanda Olivier Nduhungirehe walisaini tamko lililosimamiwa na Marekani huko Washington, huku Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio akihudhuria tukio hilo.