Muhoozi Kainerugaba: Ninamkubali Rais Samia Suluhu Hassan; 'Asante mama'
(last modified Wed, 21 May 2025 07:32:34 GMT )
May 21, 2025 07:32 UTC
  • Muhoozi Kainerugaba: Ninamkubali Rais Samia Suluhu Hassan; 'Asante mama'

Mkuu wa Majeshi ya Uganda, Jenerali Muhoozi Kainerugaba amemsifu Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kuwa ni mmoja wa viongozi anaowafadhilisha zaidi wa Afrika aliowataja kuwa "wana maamuzi makubwa".

Katika ujumbe wake wa jana Jumanne kwenye mtandao wa X, mkuu wa Jeshi la Uganda (UPDF) ambaye pia ni mtoto wa Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, alijivunia jinsi Rais Samia alivyoshughulikia kazi yake ya urais kwa mtindo "usiopenda upuuzi".

"Mama Suluhu Hassan, Rais wa Tanzania, anazidi kuwa mmoja wa viongozi ninaowapenda sana barani Afrika. Hapendi upuuzi na ni mwenye maamuzi makubwa! Asante sana, Mama" amesema Kainerugaba.

Ujumbe huo wa Jenerali Muhoozi ulionekana kuchochewa na matamshi makali ya Rais Samia baada ya Tanzania kuwazuia mawakili na wanaharakati wa Kenya kuingia nchini humo.

Aliyekuwa Jaji Mkuu wa Kenya na mtetezi wa haki za binadamu Willy Mutunga na wakili wa katiba na kiongozi wa People's Liberation Party (PLP) Martha Karua walinyimwa kibali cha kuingia Tanzania Jumapili iliyopita na baadaye wakarudishwa Nairobi.

Awali, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, alikuwa ametoa kauli kali dhidi ya kile alichokiita “uvamizi” wa wanaharakati kutoka nchi jirani, akisisitiza kuwa Tanzania haitakubali kuingiliwa katika masuala yake ya ndani.

“Tusuiwe shamba la bibi kwamba kila mtu anaweza kuja na kusema anachokitaka… Tumeanza kuona mtitiriko au mwenendo wa wanaharakati ndani ya region yetu hii, kuanza kuvamia na kuingilia mambo yetu huku,” alisema Rais Samia alipokuwa akizindua toleo jipya la Sera ya Mambo ya Nje ya mwaka 2001 (Toleo la 2024), jijini Dar es Salaam.

Rais Samia aliendelea kusisitiza kuwa Tanzania ni nchi yenye utulivu na haitaruhusu watu kutoka nje kuiingiza kwenye machafuko. “Sasa kama kwao wameshadhibitiwa wasije kutuharibia huku. 

“Niombe sana vyombo vya ulinzi na usalama na ninyi wasimamizi wa sera zetu za nje, msitoe nafasi kwa watovu wa adabu wa nchi nyingine kuja kuvuka hapa kwetu,” alisisitiza Rais Samia.

Akizungumza na wanahabari jijini Dodoma, Waziri wa Katiba na Sheria wa Tanzania, Dk. Damas Ndumbaro, alisema wanaharakati hao walikamatwa kwa sababu hawakuwa na leseni za uwakili zinazowaruhusu kushiriki katika shughuli za kisheria nchini Tanzania. Aliongeza kuwa ujio wao ulikuwa na nia ya kuvunja sheria za nchi.