Uganda yasimamisha ushirikiano wa kijeshi na Ujerumani
Jeshi la Ulinzi la Uganda (UPDF) limetangaza kusitisha kwa muda ushirikiano wa kijeshi na wa kiulinzi na Ujerumani, kutokana na mwenendo usioridhisha wa balozi wa Ujerumani nchini humo.
Msemaji wa Jeshi la Uganda, Chris Magezi, amesema katika taarifa iliyotolewa Jumapili kuwa hatua hiyo imechukuliwa kufuatia taarifa za kiusalama zenye uthibitisho kwamba Balozi Mathias Schauer anahusishwa na shughuli za kuhujumu utawala wa Uganda.
Magezi amesema: “Uamuzi wa kusimamisha ushirikiano huu utaendelea hadi pale suala la ushirikiano wa balozi huyo na vikundi vya kisiasa-kijeshi vinavyoendesha harakati za uhasama dhidi ya serikali ya Uganda litakapopatiwa suluhisho kamili."
Kupitia chapisho kwenye mtandao wa X (zamani Twitter), Mkuu wa Majeshi ya Uganda, Jenerali Muhoozi Kainerugaba, amesema kuwa changamoto iko kwa Schauer kama mtu binafsi, si kwa taifa la Ujerumani.
Kainerugaba amesema: “Tatizo ni yeye binafsi. Hana sifa zinazostahili kuwa mwakilishi hapa Uganda. Hii haina uhusiano wowote na watu wa Ujerumani ambao ni taifa kubwa na la heshima.”
Jenerali Muhoozi, ambaye pia ni mtoto wa Rais Yoweri Museveni anafahamika kwa mitazamo yake ya wazi kupitia mitandao ya kijamii ambapo mara kadhaa amebainisha wasiwasi kuhusu kuingiliwa kwa masuala ya ndani ya Uganda na mataifa ya Magharibi.
Mapema mwezi huu, aliikosoa vikali Umoja wa Ulaya (EU) kwa kile alichokiita "kucheza na moto" baada ya mabalozi wa EU kukutana na viongozi wa chama kikuu cha upinzani nchini Uganda, akiwemo kiongozi wake, mwanamuziki aliyegeuka kuwa mwanasiasa, Bobi Wine.
Wanasiasa kadhaa wa upinzani pamoja na wafuasi wao wamekamatwa kwa kuhusika na vitendo vya kuhujumu usalama wa taifa. Mwanasiasa mkongwe wa upinzani, Dkt. Kizza Besigye, kwa sasa anakabiliwa na mashtaka ya uhaini mahakamani.
Vyombo vya usalama nchini Uganda vimeonya dhidi ya juhudi zozote za kusababisha machafuko, hasa katika kipindi hiki cha maandalizi kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mapema mwaka ujao.