UN: Wakimbizi milioni 4 wametoroka vita Sudan
Umoja wa Mataifa umesema zaidi ya watu milioni 4 wamekimbia vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan.
Idadi ya watu ambao wameikimbia Sudan tangu kuanza kwa vita vyake vya wenyewe kwa wenyewe mwaka 2023 imepindukia milioni nne, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) lilisema hayo jana Jumanne na kuongeza kuwa, wengi wa walionusurika wanakabiliwa na makazi duni kutokana na uhaba wa fedha.
Msemaji wa UNHCR, Eujin Byun ameuambia mkutano na waandishi wa habari mjini Geneva kwamba, "(Vita vya Sudan vikiingia) katika mwaka wake wa tatu sasa, watu milioni 4 (kukimbia nchi) ni hatua ya kutisha, na janga kubwa zaidi la watu kuhama makazi yao katika zama hizi."
Wakati huo huo, Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) imesema kuwa, mgogoro wa kibinadamu nchini Sudan unazidi kuongezeka huku mapigano yakiendelea, watu wanazidi kuhama makazi yao na udharura wa kuchukuliwa hatua za kiafya umezidi kuwa mkubwa.
Vita hivyo vilivyoanza Aprili 2023, vimesababisha uharibifu mkubwa wa mali ya umma na miundombinu muhimu, kuua makumi ya maelfu ya watu, mbali na kulazimisha mamilioni kuwa wakimbizi ndani na nje ya Sudan.
Kamil Eltayeb Idris, Waziri Mkuu mpya wa Sudan baada ya kula kiapo siku chache zilizopita, alisisitiza kuwa atatumia muda na juhudi zake zote kwa ajili ya kudhamini maisha salama na ya heshima kwa raia wote wa nchi hiyo.