Wanamgambo wa Mai-Mai washambulia kambi ya wakimbizi mashariki mwa DRC
Wanamgambo wa Mai-Mai wameshambulia kambi moja ya wakimbizi katika mkoa wa Kivu Kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Taarifa zaidi zinasema kuwa, kambi ya wakimbizi ya Ngoroba imeshambuliwa na wanamgambo wa Mai-Mai na kisha kuchomwa moto. zaidi ya wakimbizi 500 wanapatikana katika kambi hiyo ya wakimbizi.
Wanamgambo wa Mai-Mai wamedai kuwa, wamefanya shambulio hilo kwa lengo la kuwafurusha kambini hapo waasi wa Kihutu wa Nyatura.
Baada ya shambulio hilo la wanamgambo wa Mai-Mai, wakimbizi waliokuwa katika kambi hiyo walilazimika kukimbilia maeneo ya milimani ili kuokoa maasha yao.
Wakati huo huo, waasi wa Uganda wamefanya mashambulio katika maeneo ya raia na kuwaua kwa uchache watu sita na kuwajeruhi makumi ya wengine.
Mashambulio ya waasi hao wa ADF-Nalu yamefanywa katika mkoa wa Ituri kaskazini mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imetangaza kuwa, kutokana na kushadidi mashambulio ya waasi katika maeneo mbalimbali ya mashariki mwa nchi hiyo hatua za kuimarisha zaidi usalama zimechukuliwa na serikali hiyo.
Maeneo ya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo yamekuwa yakishuhudia machafuko kwa zaidi ya miongo miwili sasa na yanahesabiwa kuwa ngome ya makundi ya waasi yanayoendesha harakati zao katika nchi hiyo.
Hayo yanajiri katika hali ambayo, raia wa mashariki mwa Congo hususan wakazi wa mkoa wa Kivu ya Kaskazini wametakiwa kujiandikisha kwa wingi katika zoezi lilioanzishwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya nchi hiyo ili wapatiwe kadi za kupigia kura kwa ajili ya uchaguzi ujao.