Kuendelea mivutano baina ya Burundi na Rwanda
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i1279-kuendelea_mivutano_baina_ya_burundi_na_rwanda
Wafuasi wa serikali ya Burundi wamefanya maandamano katika kulalamikia uingiliaji wa Rwanda wa masuala yao ya ndani. Washiriki wa maandamano hayo yaliyojiri siku ya Jumamosi na katika maeneo 119 ya Burundi walalamikia kile walichokiita kuwa ni uvamizi wa Rwanda na rais wake Paul Kagame dhidi ya nchi yao.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 15, 2016 02:53 UTC
  • Kuendelea mivutano baina ya Burundi na Rwanda

Wafuasi wa serikali ya Burundi wamefanya maandamano katika kulalamikia uingiliaji wa Rwanda wa masuala yao ya ndani. Washiriki wa maandamano hayo yaliyojiri siku ya Jumamosi na katika maeneo 119 ya Burundi walalamikia kile walichokiita kuwa ni uvamizi wa Rwanda na rais wake Paul Kagame dhidi ya nchi yao.

Baadhi ya mabango yaliyokuwa mikononi mwa waandamanaji yalikuwa yameandikwa nara zilizosema, 'Tunalaani njama za Paul Kagame za Kuibua Machafuko Nchini Kwetu.' Baada ya maandamano, waandamanaji waliekelea uliko ubalozi wa Rwanda mjini Bujumbura na kupiga nara za kupinga hatua za kichokozi za serikali ya Kigali na Rais Paul Kagame. Inaonekana kuwa, maandamano hayo yamejiri kufuatia wito uliotolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani wa Burundi, Pascal Barandagiye. Kabla ya hapo Barandagiye akizungumza kupitia televisheni ya taifa, aliwataka Warundi kushiriki kwa wingi katika maandamano ya amani kwa ajili ya kulaani uingiliaji wa Rwanda dhidi ya nchi yao. Kwa mujibu wa weledi wa mambo, inaonekana kuwa mgogoro wa kisiasa baina ya Kigali na Bujumbura unazidi kutokota. Kwa miezi kadhaa sasa Burundi imekuwa ikishuhudia hali ya mchafukoge, tangu Rais Pierre Nkurunziza wa nchi hiyo alipotangaza azma yake ya kugombea katika uchaguzi wa rais wa mwaka jana 2015, machafuko ambayo yaliambatana na mauaji. Machafuko na mauaji hayo yaliibua wasi wasi wa kuibuka kwa mara nyingine moto wa vita vya ndani nchini humo. Hata hivyo kuwepo kwa silaha nyingi mikononi mwa wapinzani, ndiko kumewafanya viongozi wa Burundi kuituhumu Rwanda kuwa inawapatia wapinzani, misaada ya kifedha, silaha na hata mafunzo ya kijeshi. Serikali ya Bujumbura inaamini kuwa, Rwanda inayaunga mkono makundi ya upinzani kwa lengo la kutaka kuiondoa madarakani serikali ya Rais Pierre Nkurunza wa nchi hiyo. Hii ni katika hali ambayo katika miezi ya hivi karibuni, Warundi wengi walikimbilia nchini Rwanda kufuatia kushadidi machafuko nchini kwao na hadi sasa bado wanaishi katika kambi maalumu za wakimbizi. Serikali ya Burundi inailaumu Kigali kwa kuwatumia vibaya wakimbizi hao katika kuwapatia mafunzo ya kijeshi kwa lengo la kuiondoa madarakani serikali ya Bujumbura. Tuhuma hizo zilisababisha Umoja wa Mataifa kuwatuma wataalamu wake kwenda nchini Rwanda kwa lengo la kuchunguza suala hilo kwa kina ambapo nao kwa kiasi fulani walithibitisha ukweli huo. Hata hivyo Rwanda kupitia Waziri wake wa Mambo ya Nje, Louise Mushikiwabo ilikadhibisha ripoti hiyo ya wataalamu wa Umoja wa Mataifa na kusisitiza kuwa, Kigali haiko tayari kuwarejesha wakimbizi hao makwao kabla ya kurejea usalama na amani nchini kwao. Hata hivyo na kinyume na matarajio, serikali ya Rwanda imetangaza azma yake ya kuwafukuza wakimbizi hao wa Burundi. Katika Kigali imetangaza kuwa, iko tayari kufanya mazungumzo na jamii ya kimataifa kuhusu namna ya kukabidhi wakimbizi wa Kirundi wapatao 75,000, kwa njia ya mwafaka na bila kuhatarisha usalama wao kwa nchi ambazo ziko tayari kuwapokea. Weledi wa mambo wanasema kuwa licha ya kwamba mgogoro baina ya Burundi na Rwanda umeongezeka hivi sasa, lakini mvutano huo wa kihistoria unaohusu tofauti za kikabila ni wa muda mrefu. Hii ni kusema kuwa, nchi mbili hizo zimekwishashuhudia vita vya ndani vya umwagaji damu mkubwa. Kwa mfano katika mauaji ya halaiki ya mwaka 1994 nchini Rwanda, zaidi ya watu laki nane wa kabila la Kitutsi waliuawa na Wahutu wenye misimamo mikali nchini humo. Huku hali ikiwa ni hivyo huko Rwanda, Burundi nayo ilishuhudia tofauti za kikaumu zilizosababisha kujiri kwa vita vya muda mrefu ambavyo viliambatana na mauaji ya maelfu ya watu nchini humo. Mvutano wa Burundi na Rwanda unajiri katika hali ambayo, kabla ya hapo, viongozi wa Umoja wa Afrika AU walikuwa wametangaza kuwa, hawako tayari kushuhudia vita vikijiri tena katika nchi za Rwanda na Burundi. Kwa mujibu wa weledi wa mambo, uingiliaji wa madola ya kigeni umekuwa chanzo cha kuibuka tofauti kubwa za kikabila katika nchi za Kiafrika, tofauti ambazo kwa kawaida huishia kuwasha moto wa vita ndani ya nchi hizo.