Wawakilishi wa Serikali ya DRC na M23 wawasili Qatar kwa mazungumzo
Wawakilishi wa serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na kundi la waasi la M23 wamewasili katika mji mkuu wa Qatar, Doha kwa mazungumzo mapana kuhusu makubaliano. Hayo yameelezwa na mwanadiplomasia mmoja anayefahamu yanayojiri kuhusu mazungumzo hayo.
"Wajumbe kutoka pande zote za DRC na ... M23 wako mjini Doha, Qatar wakiwa ndio wapatanishi wa mazungumzo hayo," amebainisha mwanadiplomasia huyo kwa sharti la kutotambulishwa kutokana na unyeti wa majadiliano.
Kundi la M23, ambalo linasemekana kuwa linaungwa mkono na Rwanda, wiki iliyopita lilitaka yafanyike majadiliano zaidi kuzungumzia matatizo ambayo hayakujumuishwa kwenye makubaliano ya amani yaliyotiwa saini kati ya Rwanda na DRC jijini Washington mwezi Juni.
"Hatua hii ya majadiliano itakuwa muhimu sana katika kufikia makubaliano," amedokeza mwanadiplomasia huyo na kuongeza kuwa wapatanishi wa Qatar wanafanya kazi ya usuluhishi kwa ushirikiano na Umoja wa Afrika.
Makubaliano yaliyofikiwa Washington kati ya DRC na Rwanda yanalenga kumaliza mapigano ambayo yamesababisha vifo vya maelfu ya watu katika eneo lenye utajiri mkubwa wa madini mashariki mwa DRC.../