Wanajeshi 4, magaidi 18 wauawa katika mapigano baada ya walinda amani wa Somalia na AU kuzima shambulio la al-Shabaab
Wanajeshi wanne wameuawa na wengine saba kujeruhiwa katika mapigano na kundi la kigaidi la al-Shabaab baada ya shambulio lao kuzimwa na jeshi la Somalia katika eneo la Lower Shabelle ambapo magaidi 18 wameuawa.
Jeshi la Somalia limezima hujuma ya wanamgambo wa al Shabaab kwa usaidizi wa wanajeshi wa kigeni walioko nchini humo.
Wizara ya Ulinzi ya Somalia imetangaza kuwa, Jeshi la Taifa la nchi hiyo (SNA) na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Uganda (UPDF), ambalo ni sehemu ya Kikosi cha Usaidizi na Kudumisha Amani cha Umoja wa Afrika nchini Somalia (AUSSOM), yamemezuia shambulio la kigaidi la al-Shabaab katika maeneo ya Sabiib na Canoole katika jimbo la Shabelle ya Chini ( Lower Shabelle) na kuua magaidi 18.
Jeshi la Somalia linaendelea na oparesheni zake za kuwasaka magaidi wa al Shabaab waliosalia huko Lower Shabelle.
Wizara ya Ulinzi ya Somalia imeripoti kuwa, wanajeshi wanne wa Jeshi la Taifa la Somalia (SNA) wameuawa na wengine saba wamejeruhiwa katika oparesheni hiyo dhidi ya magaidi wa al Shabaab.
Baada ya takriban miezi miwili ya mapigano makali, jeshi la Somalia huku likisaidiwa na vikosi vya AUSSOM, mwishoni mwa mwezi Juni mwaka huu vilivikomboa vijiji vya kimkakati vya Anole na Sabid kutoka kwa magaidi wa al-Shabaab.
Maeneo ya Anole na Sabid, yanayopatikana katika mkoa wa kusini-magharibi wa Lower Shabelle, ni maeneo ya kimkakati kwa upande wa kijeshi.