UNICEF: Watoto Sudan wanakaribia katika ukingo wa madhara yasiyoweza kurekebishwa
Kusimamishwa kwa ufadhili wa kimataifa wa fedha kunakisukuma kizazi chote cha watoto wa Sudan katika ukingo wa madhara yasiyoweza kurekebishwa huku idadi ya watoto walioathiriwa na utapiamlo nchini humo ikiongezeka. Haya ni kwa mujibu wa ripoti ya UNICEF.
Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) na mashirika mengine ya umoja huo yanakabiliwa na mojawapo ya migogoro mikubwa ya kifedha kuwahi kushuhudiwa katika miongo ya karibuni.
Akizungumza kwa njia ya video katika mji wa Port Sudan, Sheldon Yett mwakilishi wa UNICEF nchini Sudan amesema: "Watoto wanataabika na kutokana na ukosefu wa maji salama, chakula na huduma za afya. Utapiamlo umekithiri, na afya ya watoto imezorota pakubwa."
Mzozo wa Sudan kati ya jeshi la nchi hiyo na wanamgambo wa Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF) umewalazimisha mamilioni ya watu wa nchi hiyo kuwa wakimbizi na nchi hiyo kugawanyika katika maeneo mawili hasimu, huku wanamgambo wa RSF wakizidi kujikita zaidi magharibi mwa Sudan.
Mpango wa Chakula Duniani (WFP) ulisema mwezi Julai mwaka huu kuwa maeneo kadhaa ya kusini mwa mji mkuu wa Sudan, Khartoum, yako katika hatari ya kukumbwa na njaa.
Wakati huo huo Ofisi ya Kuratibu Misaada ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa imeripoti kuwa: Ni asilimia 23 tu ya mpango wa kimataifa wa misaada ya kibinadamu wa dola bilioni 4.16 kwa Sudan ambayo imetolewa hadi sasa.
Huduma za kuokoa maisha kwa watoto wa Sudan zimepungua kutokana na kusitishwa kwa baadhi ya misaada ya kifedha ya kimataifa kwa nchi hiyo.