Qatar: Tumezikabidhi DRC, M23 rasimu ya makubaliano ya amani
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i129662-qatar_tumezikabidhi_drc_m23_rasimu_ya_makubaliano_ya_amani
Qatar imetangaza habari ya kukabidhi rasimu ya makubaliano ya amani kwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na kundi la waasi la M23, ikiwa ni sehemu ya mchakato wa amani unaoendelea Doha, vyombo vya habari vya DRC viliripoti hayo jana Jumapili, vikimnukuu afisa wa Qatar.
(last modified 2025-08-18T06:44:40+00:00 )
Aug 18, 2025 06:44 UTC
  • Qatar: Tumezikabidhi DRC, M23 rasimu ya makubaliano ya amani

Qatar imetangaza habari ya kukabidhi rasimu ya makubaliano ya amani kwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na kundi la waasi la M23, ikiwa ni sehemu ya mchakato wa amani unaoendelea Doha, vyombo vya habari vya DRC viliripoti hayo jana Jumapili, vikimnukuu afisa wa Qatar.

"Ingawa muda uliowekwa katika Azimio la Kanuni za Doha la kusainiwa kwa makubaliano haukutimizwa, pande zote mbili zilijibu vyema kwa msimamizi na kuelezea nia yao ya kuendelea na mazungumzo," afisa wa Qatar aliyehusika katika juhudi za upatanishi aliiambia tovuti ya habari ya Actualite.cd.

Afisa huyo wa Qatar ameonyesha matumaini kwamba, changamoto zilizopo zinaweza kushughulikiwa "haraka" kupitia mazungumzo na "ushirikiano wa dhati" kutoka pande zote mbili.

Ikumbukwe kuwa, Julai 19, wawakilishi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na waasi wa M23 walitia saini tamko la kukubali kusitisha mapigano mashariki mwa DRC nchini Qatar.

Tamko hilo lilitiwa saini mjini Doha, mji mkuu wa Qatar, na wawakilishi kutoka pande zote mbili, kufuatia wiki kadhaa za mashauriano ya kidiplomasia, ikiwa ni pamoja na mazungumzo ya awali yaliyofanyika Washington.

Makubaliano yaliyofikiwa Washington kati ya DRC na Rwanda yalilenga kumaliza mapigano ambayo yameua maelfu ya watu katika eneo la mashariki mwa Kongo, lenye utajiri mkubwa wa madini.

Tangu mwanzoni mwa Januari 2025, waasi wa M23 wamechukua udhibiti wa maeneo kadhaa ya mashariki mwa Kongo, ikiwa ni pamoja na miji ya Goma na Bukavu, na wanaendelea kusonga mbele. 

Viongozi wa Kongo DR wainaituhumu Rwanda kwamba inawaunga mkono waasi hao, lakini serikali ya Kigali inakanusha tuhuma hizo na kusema kwamba kundi hilo linafanya kazi chini ya himaya ya serikali ya Kinshasa.