Sudan yaripoti wagonjwa wapya wa kipindupindu 1,575, vifo 22
Wizara ya Afya ya Sudan imetangaza kuwa wagonjwa 1,575 wapya wa kipindupindu na vifo 22 vimesajiliwa kote nchini humo katika muda wa wiki moja iliyopita.
Wizara hiyo imesema katika taarifa yake ya jana Jumanne kwamba jumla ya wagonjwa wanaogua kipindipindu hivi sasa imefikia 101,450 ikiwa ni pamoja na vifo 2,515.
Takwimu hizi zinajumuisha majimbo 18 ya Sudan tangu kutangazwa mlipuko wa kipindupindu nchini humo mwezi Agosti mwaka jana.
Sudan imeathiriwa na janga la kiafya huku jeshi la nchi hiyo na kikosi cha wanamgambo wa Msaada wa Haraka (RSF) wakipigana vita tangu Aprili 2023.
Watu 20,000 wameuawa na wengine milioni 14 wamelazimika kuyahama makazi yao na kutafuta hifadhi ndani na nje ya nchi.