Mwendesha mashtaka wa DRC ataka Kabila ahukumiwe kifo
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i129878-mwendesha_mashtaka_wa_drc_ataka_kabila_ahukumiwe_kifo
Mwendesha mashtaka wa kijeshi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ametoa mwito wa kutolewa hukumu ya kifo dhidi ya rais wa zamani wa nchi hiyo, Joseph Kabila ambaye mashitaka dhidi yake yanaendelea bila ya yeye kuwepo mahakamani.
(last modified 2025-10-20T07:03:11+00:00 )
Aug 23, 2025 06:15 UTC
  • Mwendesha mashtaka wa DRC ataka Kabila ahukumiwe kifo

Mwendesha mashtaka wa kijeshi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ametoa mwito wa kutolewa hukumu ya kifo dhidi ya rais wa zamani wa nchi hiyo, Joseph Kabila ambaye mashitaka dhidi yake yanaendelea bila ya yeye kuwepo mahakamani.

Jenerali Lucien Rene Likulia, mkaguzi mkuu wa hesabu za kijeshi wa Kongo, jana Ijumaa alitoa wito kwa majaji kumhukumu Kabila kifo kwa kosa la uhaini na uhalifu wa kivita, ikiwa ni pamoja na mauaji, mateso na kuandaa harakati za uasi.

Rais huyo wa zamani wa DRC alishitakiwa bila yeye kuwepo mahakamani mwezi Julai, kwa tuhuma za kuwaunga mkono waasi wa M23 wanaodaiwa kuungwa mkono na Rwanda, na ambao mwaka huu wameteka maeneo mengi yenye utajiri wa madini, mashariki mwa DRC.

Kabila, ambaye amekuwa nje ya DRC kwa miaka miwili, pia anatuhumiwa kupanga njama ya kumpindua Rais Felix Tshisekedi na mashtaka mengine ya uhalifu wa kivita yanayohusishwa na kundi la M23.

Kabila ameshutumu vikali kesi hiyo, akiitaja mahakama nchini DRC kama "chombo cha ukandamizaji". Ferdinand Kambere, katibu wa chama cha kisiasa cha Kabila, aliliambia shirika la habari la Reuters jana Ijumaa kwamba, mashitaka dhidi ya Kabila "ni katika mfululizo wa hatua za kumkandamiza mwanachama huyo wa upinzani."

Ikumbukwe kuwa, Mei mwaka huu, Kabila alikosoa vikali mfumo wa sheria wa nchi hiyo ya Afrika ya Kati, akisema kuwa umeoza na unavunda kutokana na uendeshaji mbaya. Alisema hayo muda mfupi baada ya Bunge la Seneti la nchi hiyo kumuondolea kinga ya kutoshtakiwa, na kufungua njia ya mwanasiasa huyo kufunguliwa mashtaka.