Africa CDC: Kwa muda wa wiki moja, kesi za Ebola zimeongezeka zaidi ya maradufu mkoani Kasai, DRC
Kituo cha Afrika cha Kudhibiti na Kuzuia Maradhi, (Africa CDC) kimetangaza kuwa, idadi ya watu wanaoshukiwa kuwa na ugonjwa hatari wa Ebola katika jimbo la Kasai kusini mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imeongezeka zaidi ya maradufuu katika muda wa wiki moja tangu ulipothibitishwa mripuko mpya wa ugonjwa huo katika eneo hilo.
Katika taarifa iliyotoa Alkhamisi kupitia mtandaoni, Africa CDC imesema, idadi ya kesi zinazoshukiwa imeongezeka kutoka 28 hadi 68 katika siku za hivi karibuni na kutoka wilaya mbili hadi nne, wakati idadi ya vifo kwa sasa imefikia 16.
Taarifa hiyo imeendelea kueleza kwamba, wakazi wa maeneo hayo wameingiwa na wasiwasi kutokana na mripuko huo, ambao ni kwanza nchini DRC katika kipindi cha miaka mitatu na wa kwanza katika jimbo hilo la Kasai katika kipindi cha zaidi ya muongo mmoja.
Jimbo la Kasai ni sehemu ya mbali ya Kongo DR yenye mitandao duni ya barabara na iko zaidi ya kilomita 1,000 kutoka mji mkuu wa nchi hiyo, Kinshasa.
Kwa mujibuu wa Dk. Ngashi Ngongo, mshauri mkuu wa Afrika CDC, mapigano mashariki mwa DRC yanaweza kutatiza juhudi za kukabiliana na ugonjwa wa ebola, ambao unaweza kuenea kwa kasi kutokana na ukaribu na msongamano wa vijiji na majimbo.
Mripuko mpya wa ebola ulitangazwa wiki moja iliyopita baada ya mwanamke mjamzito kuthibitishwa kuwa ameambukizwa katika mji wa Bulapé.
Kufuatia tangazo hilo, Shirika la Afya Duniani (WHO) lilituma wataalamu walioungana na Timu ya Uchukuaji Hatua za Haraka ya Kongo huko Kasai ili kutoa tiba na kufuatilia hatua za kuzuia na kudhibiti maambukizi.
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imekuwa na historia ya Ebola tangu mwaka 1976. Mripuko wa hivi karibuni ni wa 16 nchini humo na wa saba katika jimbo la Kasai. Mripuko uliopita uliozuka kati ya mwaka 2018 na 2020 mashariki mwa Kongo uliua zaidi ya watu 1,000.../