DRC: Ajali za boti zasababisha vifo vya zaidi ya watu  190
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i130734-drc_ajali_za_boti_zasababisha_vifo_vya_zaidi_ya_watu_190
Matukio mawili tofauti ya ajali wiki hii katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo yamesababisha vifo vya takriban watu 193. Makumi ya watu hawajulikani walipo huku kazi ya uokoaji ikiendelea.
(last modified 2026-02-05T09:20:29+00:00 )
Sep 13, 2025 03:38 UTC
  • DRC: Ajali za boti zasababisha vifo vya zaidi ya watu  190

Matukio mawili tofauti ya ajali wiki hii katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo yamesababisha vifo vya takriban watu 193. Makumi ya watu hawajulikani walipo huku kazi ya uokoaji ikiendelea.

Ajali hizo zilitokea Jumatano na Alhamisi katika maeneo ya kaskazini-magharibi mwa jimbo la Equateur.

Boti moja iliyokuwa na takriban abiria 500 ilipinduka baada ya kushika moto ilipokuwa ikisafiri kwenye Mto Kongo karibu na kijiji cha Malange, eneo la Lukolela, Alkhamisi jioni, Wizara ya Masuala ya Kijamii ilisema.

Katika ripoti, wizara hiyo ilisema manusura 209 wameokolewa, huku watu 146 hawajapatikana.

Boti hiyo iliteleza chini ya mkondo ilipokuwa ikiungua, ripoti ilisema, na kuongeza kuwa, moto huo uliharibu shehena ya meli hiyo na kuchoma moto  nyumba 15 kwenye ukingo wa mto.

Wanajeshi wa majini na watu waliojitolea kutoka jamii ya eneo hilo walikuwa wakisaidia katika shughuli za utafutaji na uokoaji, ambazo bado zilikuwa zikiendelea hadi jana Ijumaa.

Wakati huo huo, siku ya Jumatano, takriban watu 86 - wengi wao wakiwa wanafunzi - walikufa baada ya mashua ya injini kupinduka kwenye makutano ya mito ya Nsolo na Maringa Mkuu katika eneo la Basankusu, kulingana na vyombo vya habari vya serikali.

Watu kadhaa bado hawajapatikana, ingawa haikujulikana ni wangapi. Vyombo vya habari vya serikali vilisema manusura wanane waliokolewa kutoka majini na wakaazi wa eneo hilo.

Ajali kama hizo hutokea mara kwa mara katika Jamuri ya Kidemokrasia ya Congo na kusababisha vifo vya makumi ya watu.