Upinzani wa wanasiasa dhidi ya Rais Joseph Kabila waongezeka DRC
Hatua za wapinzani wa kisiasa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo za kupinga kuendelea kusalia madarakani Rais Joseph Kabila wa nchi hiyo zimeshtadi sambamba na kurejea nyumbani kiongozi wa upinzani mzee Étienne Tshisekedi.
Katika fremu hiyo, hivi karibuni mzee Tshisekedi, alimtimua Bruno Mavungu, mjumbe wa chama chake cha upinzani cha 'Muungano kwa ajili ya Demokrasia na Maendeleo ya Kijamii nchini Kongo DR' kwa tuhuma za kumuunga mkono Rais Kabila. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kushadidi hatua za kisiasa za wapinzani, kumeyaweka mazungumzo ya kitaifa katika hali ya kitendawili na hivyo kuongeza uwezekano wa kuzuka vita vya ndani nchini humo.
Itafahamika kuwa, hivi karibuni Rais Joseph Kabila alitoa pendekezo la kufanyika mazungumzo ya kitaifa, mazungumzo ambayo kwa muda mrefu amekuwa akiyasubiria kwa lengo la kuandaa mazingira ya kuhakikisha uchaguzi mkuu unafanyika mwaka ujao. Hata hivyo asilimia kubwa ya raia wa nchi hiyo wanayataja mazungumzo hayo kuwa ni sehemu ya mkakati wa Rais Kabila kwa ajili ya kuendelea kusalia zaidi madarakani.