Jeshi la Sudan lakabiliana na mashambulizi ya droni katika mji mkuu Khartoum
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i132920-jeshi_la_sudan_lakabiliana_na_mashambulizi_ya_droni_katika_mji_mkuu_khartoum
Jeshi la Sudan limetangaza kuwa kikosi chake cha ulinzi wa anga jana Ijumaa kilinasa kundi la ndege zisizo na rubani (droni) zilizokusudia kufanya mashambulizi katika mji wa Omdurman, magharibi mwa Khartoum, na katika mji wa kaskazini wa Atbara.
(last modified 2025-11-08T04:08:04+00:00 )
Nov 08, 2025 04:08 UTC
  • Jeshi la Sudan
    Jeshi la Sudan

Jeshi la Sudan limetangaza kuwa kikosi chake cha ulinzi wa anga jana Ijumaa kilinasa kundi la ndege zisizo na rubani (droni) zilizokusudia kufanya mashambulizi katika mji wa Omdurman, magharibi mwa Khartoum, na katika mji wa kaskazini wa Atbara.

Wakazi wa  mji wa Omdurman wameeleza kuwa walisikia sauti kubwa ya kishindi baada ya ndege kadhaa zisizo na rubani kushambulia wilaya za kaskazini mwa mji huo kabla ya mapambazuko.

Huko Atbara pia mashuhuda wamesema kuwa kundi la ndege zisizo na rubani liliushambulia mji huo kabla ya mapambazuko, na kufuatiwa na milio mikubwa ya silaha kutoka maeneo ya jeshi la Sudan. 

Hadi sasa si jeshi wala wanamgambo wa RSF waliotoa taarifa kuhusu hasara na maafa yaliyosababishwa na mashambulizi hayo. 

Chombo kimoja cha habari cha Sudan kimetangaza kuwa wanamgambo wa Kikosi cha Msaada wa Haraka  (RSF) jana walifanya mashambulizi ya ndege zisizo na rubani dhidi ya maeneo mbalimbali. 

RSF imetekeleza mashambulizi hayo ya droni huko Sudan siku moja baada ya wanagambo hao siku ya Alhamisi kusema kuwa wamekubali kufikia  usitishaji vita uliopendekezwa na Kamati ya Kimataifa ya Pande Nne. 

Taarifa iliyotolewa na wanamgambo hao wa RFS wanaotuhumiwa kutenda jinai dhidi ya binadamu huko Sudan imeeleza kuwa, wanataka usitishaji vita utekelezwe ili mchakato wa kisiasa uanze nchini humo. Aidha wanamgambo hao wamesema wamekubali kusitisha vita ili kuruhusu misaada ya kibinadamu nchini.