Maandamano yazuka Nigeria kufuatia tishio la Trump la kuivamia nchi hiyo kijeshi
Wananchi walimiminika mitaani siku ya Jumamosi katika jiji la Kano, kaskazini mwa Nigeria, kupinga vitisho vya Rais Donald Trump wa Marekani, vya kuivamia nchi hiyo kijeshi.
Waandamanaji waliokuwa na hasira walikanusha madai ya Trump kuwa eti kuna “mauaji ya Wakristo” nchini humo. Katika Jimbo la Kano, lenye idadi kubwa ya Waislamu, makundi mengi ya Kiislamu yalikusanyika kulaani vitisho vya Trump vya kuivamia Nigeria kijeshi kwa kisingizio cha kuwanusuru Wakristo.
Waandamanaji walionekana wakibeba mabango yenye ujumbe kama vile: “Tunalaani tishio la Trump kuivamia Nigeria,” “Hakuna mauaji ya Wakristo Nigeria,” na “Marekani inataka kupora rasilimali zetu,” miongoni mwa mengine. Mnamo Novemba 1, Trump alitangaza kuwa ameagiza Wizara ya Vita ya Marekani (Pentagon) kuandaa mikakati ya kijeshi dhidi ya kile alichosema ni makundi ya kigaidi nchini Nigeria kwa lengo la kuwalinda Wakristo.
Alisema kuwa endapo serikali ya Nigeria “itaendelea kuruhusu mauaji ya Wakristo,” Washington itasitisha misaada yote mara moja, na kuongeza kuwa Marekani inaweza kuivamia nchi hiyo kijeshi. Serikali ya Nigeria imekanusha vikali madai hayo, ikisisitiza kuwa hakuna “mateso ya kidini yanayoweza kuhalalishwa kwa namna yoyote ile na serikali ya Nigeria.” Waziri wa Mambo ya Nje, Yusuf Tuggar, alisema: “Katika ngazi yoyote, iwe ya kitaifa, ya kikanda, au ya mitaa, jambo hilo haliwezekani.”
Hali ya usalama nchini Nigeria inakabiliwa na changamoto kutoka kwa makundi ya kigaidi kama Boko Haram na kundi la ISIS Magharibi mwa Afrika (ISWAP), pamoja na magenge yenye silaha, makundi ya kikabila kama Watu wa Asili wa Biafra (IPOB), na migogoro kati ya wafugaji na wakulima ambayo mara nyingi hujikita katika misingi ya kiuchumi na kijamii. Weledi wa mambo wanasema kuwa lengo kuu la Trump katika vitisho vyake ni kutaka kuendelea kudhibiti sekta ya mafuta na gesi nchini humo.
Hivi karibuni, kumejiri mageuzi makubwa yanayoendelea katika sekta ya mafuta ya Nigeria, yanayoongozwa na Kiwanda cha Kusafisha Mafuta cha Dangote. Kwa mara ya kwanza katika historia ya Nigeria, nchi hiyo inajisafishia mafuta yake yenyewe. Maendeleo haya bila shaka yanapunguza utegemezi kwa mashirika ya mafuta ya Marekani. Mafanikio hayo ya Nigeria huenda yanawanyima usingizi Wamarekani.