Minawi aonya dhidi ya kugawanyika tena Sudan
-
Gavana wa Darfur, Minni Arko Minnawi
Gavana wa Darfur, Minni Arko Minnawi, ameonya kwamba makubaliano yoyote ya kusitisha mapigano nchini Sudan ambayo hayajumuishi ulinzi wa raia na kuwajibishwa wahusika wa uhalifu "yatakuwa na maana ya mgawanyiko wa Sudan," na ametoa wito wa kuondoka wale aliowaita "Janjaweed na mamluki" - akikusudia Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF)- katika maeneo ya makazi ya raia, hospitali na mijini.
Katika ujumbe wake kwenye jukwaa la X, Minnawi pia ametaka kuachiliwa watu wote waliotekwa nyara, wakiwemo watoto na wanawake, na pia kuhakikisha watu waliokimbia makazi yao wanarejea makwao.
"Kusitishwa mapigano bila ya mpango wa kuwalinda raia na kuwawajibisha wahusika wa uhalifu kuna faida gani? Makubaliano yoyote ya amani bila mambo haya yanamaanisha mgawanyiko wa Sudan", amesema Gavana wa Darfur, Minni Arko Minnawi.
Katika muktadha huo, Mkurugenzi wa Ofisi ya Utendaji ya Tume ya Misaada ya Kibinadamu katika Jimbo la Khartoum, Al-Fadil Mubarak, ametangaza kwamba zaidi ya watu 10,000 waliokimbia makazi yao wamewasili katika Jimbo la Khartoum kutokana na mashambulizi ya Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) katika maeneo ya Kaskazini mwa Darfur na Kaskazini mwa Kordofan.
Mubarak ametoa wito kwa mashirika ya kibinadamu kutoa msaada wa haraka kwa watu hao waliolazimika kuhama makazi yao, hasa misaada ya kukabiliana na msimu wa baridi ambao umeanza nchini Sudan, pamoja na vifaa vya usafi na dawa.
Sudan imekuwa katika vita kati ya Jeshi la Taifa na Vikosi vya Msaada wa Haraka tangu Aprili 2023, ambavyo vimesababisha mauaji ya makumi ya maelfu ya watu, na kuwalazimisha wengine milioni 13 kuhama makazi yao.