IRGC yavunja mtandao wa udukuzi unaohusishwa na Mossad
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i133018-irgc_yavunja_mtandao_wa_udukuzi_unaohusishwa_na_mossad
Shirika la Ujasusi la Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) limetangaza mafanikio makubwa ya kukabiliana na ujasusi, na kumkamata kiongozi wa kundi la udukuzi linalojulikana kama "Backdoor."
(last modified 2025-11-10T12:12:12+00:00 )
Nov 10, 2025 12:12 UTC
  • Iran yasambaratisha mtandao wa ujasusi wa Israel
    Iran yasambaratisha mtandao wa ujasusi wa Israel

Shirika la Ujasusi la Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) limetangaza mafanikio makubwa ya kukabiliana na ujasusi, na kumkamata kiongozi wa kundi la udukuzi linalojulikana kama "Backdoor."

Kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari vya Iran, kiongozi wa kundi hilo alifanya kazi kwa kutumia jina bandia la msichana Mholanzi akidai kutetea uhuru wa wanawake wa Iran, na inasemekana alikuwa akitoa taarifa za siri kuhusu vikosi vya usalama vya Iran kwa mitandao ya vyombo vya habari vinavyopinga Jamhuri ya Kiislamu, ikiwa ni pamoja na Iran International, na mitandao iliyounganishwa na shirika la ujasusi la Israel, Mossad.

Kesi hiyo ilianza mwaka wa 2022 wakati chaneli ya Telegram ya "Backdoor" na akaunti ya Twitter ilipopata umaarufu kwa kuchapisha taarifa binafsi kuhusu maafisa wa polisi wa maadili na wanajeshi wengine wa Iran.

Hapo awali, "Backdoor" alijitambulisha kama mwanamke kijana wa Ulaya eti anayefichua siri za kuwaunga mkono wanawake wa Iran. Simulizi hii ilitiwa chumvi na kukuzwa sana na vyombo vya habari vya kigeni.

Hata hivyo, operesheni ya ujasusi yenye tabaka nyingi iliyofanywa na wataalamu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (IRGC) ilionyesha kuwa mhusika hakuwa "msichana" wala "Mholanzi," bali ni kijana wa Iran aliyeongoza kundi la udukuzi wa ndani ya nchi.

Kwa mujibu wa maungamo yake, nia yake kuu ilikuwa kupata pesa kupitia sarafu ya kidijitali.

Kiongozi wa kundi hilo aliyekamatwa amekiri kupokea malipo mkabala wa malengo maalumu na kutoa taarifa zenye thamani kubwa.

Esmaeil Fekri, amenyongwa kwa kupatikana na hatia ya kufanya kazi na shirika la ujasusi la Mossad.

Uchunguzi umegundua kuwa kundi hilo la udukuzi lilikuwa sehemu ya mtandao mpana na hatari zaidi unaowahusisha waandishi wa habari wa mtandao wa 'Iran International', kundi pinzani la udukuzi "Lab Dookhtegan" na hatimaye, shirika la ujasusi la Israel, Mossad.

Kundi la "Lab Dookhtegan" linajulikana kwa mwelekeo wake wa wazi wa kuunga mkono Wazayuni na lilijivunia kwenye chaneli yake ya Telegram kuhusu nafasi yake katika kukusanya malengo ya kijasusi ndani ya Iran wakati wa migogoro ya hivi karibuni.

Vyombo vya usalama vya Iran vinaweka kipaumbele kikubwa katika kugundua na kusambaratisha shughuli za ujasusi wa kigeni.

Mara nyingi, operesheni hizo hulenga mitandao inayoendeshwa na CIA na Mossad.