Mkutano mkubwa wa wapinzani wa serikali ya Zimbabwe katika mji mkuu Harare
Viongozi wa mrengo wa upinzani unaoipinga serikali ya Zimbabwe wamekusanyika katika mji mkuu wa nchi hiyo Harare na kufanya mkutano mkubwa uliowajumuisha wafuasi wa vyama vya upinzani.
Morgan Tsvangirai Kiongozi wa chama cha Mabadiliko ya Demokrasia (MDC) ameungana pamoja na Bi Joyce Mujuru Makamu wa zamani wa Rais Robert Mugabe kulalamikia hatua ya rais huyo ya kusalia madarakani. Viongozi hao wawili wametaka kuuungana vyama vyote vya upinzani ili kuiongoza Zimbabwe.
Joyce Mujuru mwezi Machi mwaka huu aliasisi chama kwa jina la "Zimbabwe People First" na kisha akajiunga na mrengo wa upinzani. Joyce ni mke wa hayati Jenerali Mujuru, mpigania uhuru mashuhuri wa Zimbabwe na alifukuzwa kwenye chama tawala Zanu-Pf mwaka 2014. Kabla ya kuuzuliwa wadhifa wake na Rais Robert Mugabe, Bi Joyce Mujuru alikuwa akitajwa sana katika duru za kisiasa kuwa chaguo sahihi aliyestahiki kuchukua nafasi ya Rais wa baadaye wa Zimbabwe. Weledi wa mambo wanaamini kuwa sababu iliyopelekea kuuzuliwa wadhifa wa Makamu wa Rais Bi Joyce Mujuru ni kutokana na vita vya kuwania madaraka vilivyopo ndani ya chama tawala cha Zanu-Pf.
Hii ni katika hali ambayo kuwepo mivutano na miganyiko kati ya vyama vya upinzani na wale wanaomkosoa Rais Robert Mugabe, ni moja ya sababu zinazompa ushindi mara zote Rais Mugabe. Hata hivyo hivi sasa masuala hayo yote yanaonekana kutoweka. Tukio jipya limejiri huko Zimbabwe sasa baada ya kudhihiri Harakati ya Wananchi kwa jina la " This Flag Movement", chini ya uongozi wa Mchungaji Evan Mawarire, huku sauti za pamoja za wananchi zikisikika katika pembe mbalimbali za nchi hiyo. Morgan Tsvangirai pia ambaye kwa mara nyingine alishindwa mbele na Mugabe katika uchaguzi wa Rais wa Agosti mwaka 2013 kwa kupata asilimia 34 ya kura, ana matarajio kuwa harakati hiyo ya wananchi na wapinzani wa Zimbawe mara hii itafanikiwa kushika dola.
Morgan Tsvangirai ambaye baada ya kushindwa katika uchaguzi mwaka 2008 aliweza kwa mara ya kwanza kushirikishwa katika muundo wa serikali ya mseto na chama tawala, hivi sasa ameazimia kuibua harakati ya wapinzani wa kisiasa wa Robert Mugabe. Mugabe ambaye amezungumzia wazi nia yake ya kuwania tena katika uchaguzi wa mwaka 2019, bado hajamuarifisha shakhsia yoyote atakayekiongoza chama tawala cha Zanu-Pf. Wakati huo huo, mgogoro wa kiuchumi unaoikabili Zimbabwe umeifanya serikali ishindwe kuwalipa mishahara wafanyakazi wa serikali na polisi ya nchi hiyo. Mwezi Juni mwaka huu, serikali ya Harare iliweza kuwalipa mishahara askari polisi peke yao, na mwezi Julai pia, ucheleweshwaji wa mishahara hiyo ulisababisha mgomo na maandamano ya nchi nzima dhidi ya serikali katika mji mkuu Harare na katika baadhi ya miji mikubwa ya Zimbabwe. Hii ni katika hali ambayo ulipaji mishahara ya wafanyakazi ya mwezi Agosti pia imeakhirishwa kwa wiki moja.
Katika mazingira kama hayo, kushiriki viongozi wa vyama viwili vya upinzani katika mkutano wa wafuasi wao huko Harare ambao wamewatolea wito wananchi kuwa na umoja na mshikamano dhidi ya Mugabe, kunatishia nafasi ya rais huyo ambaye amekuwa uongozini kwa muda wa miongo mitatu. Weledi wa masuala ya kisiasa wanaamini kuwa kuungana vyama vya upinzani na wakosoaji wakuu wa Rais Robert Mugabe kutasaidia kuleta nguvu kwa ajili ya kuusambaratisha udikteta katika uchaguzi ujao wa rais huko Zimbabwe.