Wagombea kiti cha urais Gabon waungana
Wagombea wa kiti cha urais nchini Gabon wanaoipinga serikali ya nchi hiyo wameamua kuungana ili kuibuka na ushindi katika uchaguzi ujao wa rais.
Guy Nzouba Ndama Spika wa zamani wa bunge la Gabon na Casimir Oye-Mba Waziri Mkuu wa zamani wa nchi hiyo wameamua kuungana na Jean-Ping mshindani mkuu wa Rais Ali Bongo ili kumbwaga rais huyo katika uchaguzi ujao wa rais. Muungano huo wa wagombea wa kiti cha urais unatazamia kutangazwa rasmi baadaye hii leo. Waziri Mkuu wa zamani wa Gabon amesema kuwa wameamua kuungana na wagombea wengine kwa maslahi ya taifa.
Hayo yanajiri katika hali ambayo zimebaki siku 12 tu hadi kufanyika uchaguzi wa rais huko Gabon huku kampeni za wagombea zikianza rasmi tangu wiki iliyopita.
Akizungumza siku kadhaa zilizopita katika mahojiano na jarida la wiki la African Youth, Rais Ali Bongo alivituhumu vyama vinavyoipinga serikali kuwa vinachochea machafuko ya kisiasa katika kukaribia uchaguzi wa rais. Wapinzani nchini Gabon wanaamini kuwa upo uwezekano uchaguzi ujao wa rais nchini humo ukagubikwa na udanganyifu.