Waasi wa ADF wafanya tena mashambulio mashariki mwa DRC
Waasi wa ADF-NALU wa Uganda wameendelea kufanya mashambulio katika maeneo mbalimbali ya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Omar Kavota, msemaji wa makundi ya kiraia katika Jimbo la Kivu Kaskazini amesema kuwa, raia watatu waliuawa jana katika kijiji kimoja kwenye mji wa Beni ulioko katika mkoa wa Kivu Kaskazini baada ya waasi wa uganda wa ADF-NALU kufanya mashambulio katika maeneo hayo.
Omar Kavota amesema kuwa, shambulio hilo lilifanyika kwa lengo la kudhoofisha ari ya jeshi la Congo DRC katika operesheni zake dhidi ya makundi yanayobeba silaha mashariki mwa nchi hiyo.
Shambulio hilo limeafanyika siku chache tu baada ya waasi hao wa Uganda kufanya mashambulio makubwa Jumamosi iliyopita katika mji wa Beni na kupelekea kwa uchache raia 51 kuuawa na makumi ya wengine kujeruhiwa.
Ripoti zinaeleza kuwa, hali ya usalama katika mji wa Beni imezidi kuwa mbaya katika siku za hivi karibuni kutokana na kushadidi mashambulio ya makundi ya waasi katika mji huo. Raia wengi wa mji huo wamekuwa wakiyakimbia makazi yao ili kusalimisha maisha yao.
Eneo la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo limekuwa likishuhudia machafuko kwa zaidi ya miaka 20 sasa kutokana na kuwa ngome ya makundi kadhaa ya waasi kutoka nchi jirani za Rwanda na Uganda.
Baadhi ya vijiji vya mashariki mwa nchi hiyo vinadhibitiwa na makundi ya waasi hali ambayo imewafanya wakazi wake kuyaacha makazi yao na kuwa wakimbizi.