Wakazi wa Beni watakiwa kushirikiana na jeshi la Kongo
Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imewataka wakazi wa mji wa Beni nchini humo kushirikiana na jeshi katika mapambano dhidi ya makundi yenye silaha.
Lambert Mende-Omalanga Msemaji wa serikali ya Kongo amesema upashanaji taarifa una nafasi kuu katika mapambano dhidi ya makundi yenye silaha na kwamba raia wanapasa kuwapa taarifa askari usalama kuhusu tukio lolote linalojiri katika makazi yao.
Lambert Mende-Omalanga amesema kuwa Baraza Kuu la Ulinzi la Kongo limeainisha hatua za kuchukuliwa kwa lengo la kuyaangamiza makundi yenye silaha katika mji wa Beni mkoani Kivu ya Kaskazini kwa ufanisi zaidi. Hatua hizo zimechukuliwa katika kikao kilichofanywa na baraza hilo katika mji wa Goma makao makuu ya mkoa wa Kivu ya Kaskazini huko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Mende ameongeza kuwa hatua hizo za kiusalama zimechukuliwa lengo likiwa ni kuimarisha ubadilishanaji taarifa kati ya raia na askari usalama. Watu zaidi ya 650 wameuawa tangu mwezi Oktoba mwaka juzi hadi hivi sasa katika mji wa Beni mashariki mwa Kongo na katika maeneo ya karibu na mji huo katika mashambulizi mbalimbali ya makundi ya wabeba silaha.