Kenya yatathmini kutuma wanajeshi Sudan Kusini
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i13540-kenya_yatathmini_kutuma_wanajeshi_sudan_kusini
Bunge la Kenya linatazamiwa kujadili hoja ya iwapo serikali ya Nairobi itatuma wanajeshi wa nchi hiyo KDF nchini Sudan Kusini au la, wiki moja baada ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kupasisha azimio la kutumwa askari 4,000 zaidi nchini humo.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Aug 19, 2016 02:52 UTC
  • Kenya yatathmini kutuma wanajeshi Sudan Kusini

Bunge la Kenya linatazamiwa kujadili hoja ya iwapo serikali ya Nairobi itatuma wanajeshi wa nchi hiyo KDF nchini Sudan Kusini au la, wiki moja baada ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kupasisha azimio la kutumwa askari 4,000 zaidi nchini humo.

Jana Alkhamisi, Adan Duale, kiongozi wa kambi ya serikali Bungeni aliwasilisha hoja hiyo maalumu na kuitaja kuwa ni ya dharura na yenye umuhimu mkubwa sio tu kwa Sudan Kusini bali kwa eneo zima. Alisema kuwa amani na uthabiti katika nchi hiyo changa zaidi barani Afrika ni kwa maslahi ya nchi zote za kanda ya Afrika Mashariki na Kati.

Adan Duale, kiongozi wa kambi ya serikali katika Bunge la Kenya

Umoja wa Mataifa umepongeza hatua ya Sudan Kusini kukubali pendekezo la kutumwa askari wa kieneo nchini humo kufuatia mapigano ya ndani kati ya askari watiifu kwa Rais Salva Kiir na wafuasi wa aliyekuwa makamu wake, Riek Machar, ambapo mamia ya watu wameuawa na makumi ya maelfu ya wengine kulazimika kuwa wakimbizi.

Wiki mbili zilizopita, jumuiya ya kikanda ya IGAD baada ya kufanya mkutano wa dharura mjini Addis Ababa, Ethiopia, ilitangaza kuwa, serikali ya Juba imekubali pendekezo la kutumwa askari wa nchi za kieneo nchini humo.

Askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa Sudan Kusini

Suala la kutumwa askari wa nchi kadhaa za Afrika nchini Sudan Kusini ni miongoni mwa matakwa yaliyotolewa na Riek Machar ambaye aliukimbia mji wa Juba baada ya kushadidi mapigano na ambaye kwa sasa imearifiwa kuwa ameitoroka nchi kwa madai kuwa anaandamwa na askari watiifu kwa Rais Salva Kiir.