Besigye: Uchaguzi ujao hautakuwa huru na wa amani
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i1366-besigye_uchaguzi_ujao_hautakuwa_huru_na_wa_amani
Mgombea urais katika uchaguzi ujao nchini Uganda na mwanasiasa ambaye anahesabiwa kuwa mpinzani mkuu wa Rais Yoweri Museveni, amelaani ukandamizaji wa jeshi la polisi dhidi ya wafuasi wa kambi ya upinzani na kusema kuwa, mwenendo huo haufai.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 16, 2016 11:32 UTC
  • Besigye: Uchaguzi ujao hautakuwa huru na wa amani

Mgombea urais katika uchaguzi ujao nchini Uganda na mwanasiasa ambaye anahesabiwa kuwa mpinzani mkuu wa Rais Yoweri Museveni, amelaani ukandamizaji wa jeshi la polisi dhidi ya wafuasi wa kambi ya upinzani na kusema kuwa, mwenendo huo haufai.

Dakta Kizza Besigye ameyasema hayo hii leo baada ya mwanachama mmoja wa upinzani kuuawa na polisi ya nchi hiyo. Sanjari na kuthibitisha habari ya mauaji hayo, amesema kuwa hana matumaini ya kufanyika uchaguzi wa siku ya Alkhamisi katika mazingira ya uhuru na uwazi.

Naye Msemaji wa Jeshi la Polisi la Uganda, Fred Ananga amethibitisha habari ya kuuawa mwanachama huyo wa upinzani na kuongeza kuwa, mtu huyo aliuawa katika vurugu na askari wa jeshi hilo. Ananga amesema kuwa, katika vurugu hizo polisi walitumia pia mabomu ya kutoa machozi na risasi bandia kwa ajili ya kuwatawanya waandamanaji.

Polisi ya Uganda imemzuia Dakta Kizza Besigye kufanya mikutano kadhaa ya kampeni suala ambalo limelaaniwa vikali na kinara huyo wa chama kikuu cha upinzani. Uchaguzi mkuu nchini Uganda utafanyika tarehe 18 Februari, yaani siku ya Alkhamisi ijayo. Rais Museven amekuwa madarakani kwa kipindi cha miaka 30 sasa.