Mrengo wa upinzani DRC wakataa mazungumzo na serikali ya Rais Joseph Kabila
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i13696-mrengo_wa_upinzani_drc_wakataa_mazungumzo_na_serikali_ya_rais_joseph_kabila
Muungano wa upinzani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo umekataa kufanya mazungumzo na serikali ya Rais Joseph Kabila kuhusiana na suala la uchaguzi ambao sasa imetangazwa kuwa, utafanyika Julai mwakani badala ya mwezi Novemba mwaka huu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 21, 2016 10:40 UTC
  • Mrengo wa upinzani DRC wakataa mazungumzo na serikali ya Rais Joseph Kabila

Muungano wa upinzani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo umekataa kufanya mazungumzo na serikali ya Rais Joseph Kabila kuhusiana na suala la uchaguzi ambao sasa imetangazwa kuwa, utafanyika Julai mwakani badala ya mwezi Novemba mwaka huu.

Mrengo wa upinzani umetangaza kuwa, utaitisha mgomo mkubwa Jumanne ijayo kupinga kuakhirishwa uchaguzi wa Rais.

Wapinzani hao wanamtaka Rais Kabila achie ngazi na kuondoka madarakani Disemba mwaka huu kama inavyoagiza katiba ya nchi. Hata hivyo, Tume ya Uchaguzi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imetangaza kuahirishwa uchaguzi wa rais nchini humo hadi mwezi Julai 2017 ikisisitiza kwamba, muda uliobakia hadi Novemba mwaka huu hautoshi kuendesha zoezi la uchaguzi.

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Kongo amesema kuwa, shughuli ya uandikishaji majina ya wapiga kura iliyoanza mwezi Machi mwaka huu, itahitajia muda wa miezi 16 hadi kukamilika.

Awali Mahakama Kuu ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ilitangaza kuwa iwapo itashindikana kuanda uchaguzi wa rais katika wakati ulioainishwa basi Rais Kabila anaweza kubakia madarakani hadi wakati wa kufanyika uchaguzi mkuu. 

Étienne Tshisekedi, kiongozi mkongwe wa upinzani DRC

Taarifa ya upinzani iliyochapishwa katika tovuti yake inasema kama ninavyonukuu: Vyama vya upinzani vinawataka wananchi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kushiriki katika mgomo mkubwa tarehe 23 Agosti.

Aidha wapinzani wa nchi hiyo wamemtuhumu Edem Kodjo mpatanishi wa Umoja wa Afrika katika mgogoro wa DRC kwamba, anaipendelea serikali na wametaka ajiuzulu nafasi yake hiyo.

Rais Kabila alishika hatamu za kuiongoza Kongo mwaka 2001 baada ya kuuawa baba yake, Laurent Kabila, na kisha akashinda uchaguzi wa rais uliofanyika mwaka 2006. Kwa mujibu  wa katiba ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Rais Joseph Kabila haruhusiwi kugombea tena kiti hicho baada ya kuhudumu kwa vipindi viwili vya miaka mitano mitano.