Sudan: Ni matumaini yetu amani itapatikana karibuni hivi Sudan Kusini
Waziri wa Habari wa Sudan amesisitizia wajibu wa kufanywa juhudi za makusudi za kukomesha mapigano ya silaha nchini Sudan Kusini na kutatuliwa mgogoro wa nchi hiyo kwa njia ya mazungumzo.
Ahmad Bilal Othman amesema hayo leo na kuongeza kwamba, Khartoum ina matumaini kuwa mgogoro wa kisiasa nchini Sudan Kusini utapatiwa ufumbuzi karibuni hivi.
Aidha amesema, hivi sasa mkuu wa waasi wa Sudan Kusini, Riek Machar yuko nchini Sudan kwa matibabu.
Ni vyema kusema hapa kuwa, baada ya kuzuka mapigano makali ya umwagaji wa damu baina ya wafuasi wa Riek Machar na wale wa Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini mjini Juba kuanzia tarehe 8 hadi 11 mwezi uliopita wa Julai, Riek Machar aliondoka Juba na kukimbilia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Tangu yalipozuka mapigano hayo hadi hivi sasa, hali ya usalama bado haijawa nzuri mjini Juba. Mapigano ya mara kwa mara na ya hapa na pale yamekuwa yakiripotiwa kutokea baina ya wafuasi wa Rais Salva Kiir na makamu wake wa zamani, Riek Machar.
Hadi sasa watu 270 wameshauawa na maelefu ya wengine kuyakimbia makazi yao kutokana na mapigano hayo.