Wanajeshi wanne wa Chad wauawa mpakani na Niger
Wanajeshi wanne wa Chad wameuawa baada ya kuripuka bomu la kutegwa ardhini katika eneo moja la mpakani mwa nchi hiyo na Niger.
Duru za usalama za Chad zilitangaza habari hiyo jana (Jumamosi) na kusema kuwa, wanajeshi hao wanne wameuawa baada ya gari walilokuwa wakisafiria kukanyaga bomu la kutegwa ardhi katika eneo la Kaiga linalopakana na Niger.
Maafisa usalama wa serikali ya Chad wameelekeza kidole cha lawama kwa wanamgambo wa Boko Haram na kuongeza kuwa, wanajeshi wengine 10 wamejeruhiwa kwenye tukio hilo. Askari waliojeruhiwa wamepelekwa N'Djamena, mji mkuu wa nchi hiyo.
Kundi la Boko Haram lilianzisha mashambulizi ya kigaidi mwaka 2009 nchini Nigeria na mwaka 2015 likapanua mashambulizi yake hadi katika nchi jirani za Chad, Niger na Cameroon.
Hadi hivi sasa maelfu ya watu wameshauawa, kuwa wakimbizi na kujeruhiwa kutokana na mashambulizi ya genge la kigaidi la Boko Haram kwenye eneo hilo la magharibi mwa Afrika.
Taathira mbaya za mashambulizi ya Boko Haram zimewadhuru zaidi wanawake na watoto wadogo huku Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF) ukitangaza kuwa, robo ya mashambulizi ya kigaidi ya kundi hilo yanafanywa na watoto.
Mkurugenzi wa Unicef katika kanda ya magharibi na katikati mwa Afrika, Manuel Fontaine amesema kuwa, watoto 38 wametumiwa na kundi la Boko Haram kufanya mashambulizi ya kijiripua kwa mabomu tangu mwanzoni mwa mwaka huu wa 2016 na 86 wametumiwa kujiripua kwa mabomu tangu mwaka 2014 hadi sasa katika eneo la Ziwa Chad linalozijumuisha nchi za Nigeria, Niger, Chad na Cameroon.