Waasi wa Mai Mai waua raia wawili mashariki mwa Kongo
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i14224-waasi_wa_mai_mai_waua_raia_wawili_mashariki_mwa_kongo
Watu wawili wameuliwa baada ya watu wenye silaha kukishambulia kijiji kimoja mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 29, 2016 23:30 UTC
  • Waasi wa Mai Mai waua raia wawili mashariki mwa Kongo

Watu wawili wameuliwa baada ya watu wenye silaha kukishambulia kijiji kimoja mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Afisa mmoja katika eneo la Lubero kaskazini mwa mkoa wa Kivu ya Kaskazini mashariki mwa Kongo amesema kuwa wanamgambo wa Mai Mai usiku wa Jumapili kuamkia Jumatatu walikivamia kijiji cha Chuto ambacho wakazi wake wengi ni wa kabila la Hutu na kuuwa raia wawili, ambao wametambuliwa kuwa ni mwanamke na mtoto mmoja. Wakazi wengine saba wa kijiji hicho wamejeruhiwa katika uavmizi huo wa wanamgambo wa Mai Mai.

Kijiji cha Chuto kilichoshambuliwa na Wanamgambo wa Mai Mai katika eneo la Lubero mashariki mwa Kongo DR

Kijiji cha Chuto kipo umbali wa kilomita 260 kaskazini mwa mji wa Goma katika mpaka wa Butembo. Mamia ya watu wameuawa katika mapigano ya kikabila yaliyojiri kati ya makabila mawili ya Nande na Hutu tangu kuanza mwaka huu wa 2016. Itakumbukwa kuwa watu saba waliuawa katika mapigano yaliyojiri tarehe Nane mwezi huu kati ya makabila hayo mawili huko Lubero.