Wanigeria wakaribisha azma ya serikali kutaka kuzungumza na Boko Haram
Taasisi tofauti za kijamii na kiutamaduni nchini Nigeria zimekaribisha azma ya serikali juu ya kufanya mazungumzo na wanachama wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram kuhusiana na hatima ya wanafunzi wa kike wanaoshikiliwa na genge hilo.
Taarifa iliyotolewa na taasisi hizo imesema kuwa, uamuzi wa serikali ya Abuja kwa ajili ya kulipatia ufumbuzi suala la watoto hao wa kike, unaashiria azma ya dhati ya serikali hiyo kwa ajili ya kupambana na uasi na machafuko nchini. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, endapo wanamgambo wa Boko Haram watakuwa wakweli na kutekeleza ahadi, kutakuwa na uwezekano wa kuachiliwa huru wasichana hao wa shule ya msingi ambao wamekuwa wakishikiliwa tangu mwaka 2014 hadi sasa.
Kwa upande wake Muhammad Askira, katibu wa muungano wa asasi za kiraia nchini Nigeria amekaribisha juhudi za jeshi katika mapambano yake ya kulitokomeza kundi la Boko Haram. Itakumbukwa kuwa tarehe 14 mwezi Aprili mwaka 2014, wanachama wa genge hilo walivamia shule ya msingi ya mji wa Chibok jimbo la Borno na kuwateka nyara wasichana wa kike 276. Hivi karibuni Rais Muhammadu Buhari wa nchi hiyo alinukuliwa akisema kuwa serikali yake inapendelea kufanya mazungumzo na wanachama wa genge hilo kwa lengo la kuachiliwa huru mabinti hao. Baadhi ya weledi wa mambo waliyataja matamshi ya rais huyo kama aina fulani ya kukiri kushindwa jeshi lake katika kukabiliana na magaidi hao.