WHO yaonya kuhusu kuenea Kipindupindu kaskazini mwa DRC
Shirika la Afya Duniani (WHO) limeonya kuhusu kuenea mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu huko Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo.
Katika taarifa yake ya leo Ijumaa, WHO imesema mara nyingi mlipuko huo husalia mashariki mwa nchi hiyo lakini sasa hivi umeenea hadi katika mji mkuu Kinshasa na kufanya idadi ya waliopatwa na kipindupindu hadi sasa mwaka huu DRC kufikia elfu 18, idadi ambayo ilikuwa ya mwaka mzima uliopita.
Dokta Dominique Legros kutoka WHO amewaeleza wanahabari mjini Geneva, Uswisi kuwa tayari hatua zimeanza kuchukuliwa kusaidia Wizara ya Afya na wadau ikiwa ni pamoja na kupeleka wataalamu na vifaa vya tiba. Ameongeza kuwa WHO itasaidia kampeni ya kutoa chanjo huko Kinshasa mwisho wa mwezi, ikilenga watu laki tatu.
Amebaini kuwa lengo la kampeni hiyo ambayo inalenga maeneo hatarini zaidi ya Kinshasa ambao ni mji mkubwa wenye watu Milioni Tano, ni kudhibiti mlipuko na kuepusha janga kama la miaka mitano iliyopita ambapo visa vilikuwa vingi, halikadhalika vifo.