Jeshi laua waasi 20 mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i14896-jeshi_laua_waasi_20_mashariki_mwa_jamhuri_ya_kidemokrasia_ya_kongo
Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo limetangaza kuua idadi kadhaa ya waasi mashariki mwa nchi hiyo.
(last modified 2026-04-29T03:42:39+00:00 )
Sep 08, 2016 09:43 UTC
  • Jeshi laua waasi 20 mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo

Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo limetangaza kuua idadi kadhaa ya waasi mashariki mwa nchi hiyo.

Taarifa iliyotolewa leo na jeshi la nchi hiyo imesema kuwa, katika operesheni maalumu za jeshi dhidi ya waasi wanaoitwa 'Wapiganaji wa Umoja wa Kidemokrasia' zilizofanyika katika mkoa wa Kivu Kaskazini, mashariki mwa nchi hiyo, eneo la mpaka wa pamoja na Rwanda, jumla ya waasi 20 wameuawa. Kwenye ripoti hiyo pia jeshi la nchi hiyo limesisitiza kuwa, katika operesheni hizo waasi wengine 25 wametiwa mbaroni sambamba na kudhibiti idadi kubwa ya silaha zao.

Maandamano mjini Kinshasa

Hii ni katika hali ambayo siku chache zilizopita mji wa Kinshasa, mji mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ulishuhudia wimbi la maandamano dhidi ya serikali ya Rais Joseph Kabila. Wapinzani wanaituhumu serikali na maafisa usalama wa nchi hiyo kwa kushindwa kukabiliana na waasi na makundi ya wabeba silaha sanjari kabisa na kushindwa kwao kulinda raia wa kawaida. Aidha wiki iliyopita wakazi wa mji wa Beni, katika mkoa wa Kivu Kaskazini sanjari na kufanya maandamano makubwa dhidi ya serikali waliitaka serikali hiyo kuchukua hatua za haraka kwa ajili ya kurejesha usalama na amani eneo hilo.