Watu kadhaa wajeruhiwa katika mashambulizi mapya DRC
-
Askari wa kofia buluu wa Umoja wa Mataifa nchini Kongo
Watu wenye silaha wamefanya mashambulizi katika eneo la kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na kujeruhi watu watatu.
Duru za kuaminika za nchi hiyo zimetangaza habari hiyo na kuwataja watu waliojeruhiwa kuwa ni afisa mmoja wa mahakama ya kijeshi katika mji wa Bunia, makao makuu ya mkoa wa Ituri, afisa mmoja wa polisi katika eneo la Mungwalu, huko huko Ituri, na raia mmoja aliyeshambuliwa na watu wenye silaha waliokuwa garini katika eneo la baina ya Bunia na Mahagi, mkoani Ituri.
Wanaharakati wa asasi za kijamii wanawatuhumu baadhi ya wanajeshi wa nchi hiyo kuwa ndio wanaofanya uvujifu wa amani. Hata hivyo jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo limekanusha madai hayo na kusema kuwa, jeshi hilo lipo kwa ajili ya kulinda amani, na si kusababisha machafuko na ukosefu wa usalama.
Carlos Kalombo Kenga ni msemaji wa jeshi la DRC mkoani Ituri. Amesema, watu wasiojulikana wenye silaha wanafanya uhalifu kwa kutumia fursa ya kutoka wanajeshi wa nchi hiyo kwa ajili ya kufanya doria.
Aidha ameahidi kufuatiliwa na kupewa adhabu kali mwanajeshi yeyote atakayegundulika anatumia nguvu kufanya uhalifu dhidi ya raia.
Hadi hivi sasa jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na askari wa kofia buluu wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa wameshindwa kumaliza uasi katika maeneo ya mashariki mwa nchi hiyo na hadi leo vitendo vya kihalifu vinaripotiwa mara kwa mara kwenye eneo hilo.