Wanajeshi 7 wa Niger wauawa na kundi la kigaidi la Boko Haram
Jeshi la Niger limetangaza kuwa, wanajeshi wake saba wameuawa kusini mashariki mwa nchi hiyo kufuatia mashambulio la wanamgambo wa kundi la kigaidi la Boko Haram.
Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Niger ametangaza kuwa, wanajeshi hao wameuawa katika shambulio la kuvizia la wanamgambo wa Boko Haram katika kijiji cha Toumour yapata kilomita 75 kaskazini mwa mji wa Diffa ulioko kusini mashariki mwa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.
Wakati huo huo, wanajeshi wengine wawili wa Niger waliuawa siku ya Alkhamisi baada ya gari lao kulipuka wakati walipokuwa katika doria kwenye eneo la Baroua.
Katika miaka ya karibuni, mashambulio ya kundi la Boko Haram ambalo ngome yake kuu iko katika eneo la kaskazini mashariki mwa Nigeria yamezilenga pia nchi jirani za Chad, Cameroon na Niger.
Zaidi ya watu 30,000 wameuawa hadi sasa nchini Nigeria kutokana na mashambulio ya kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram, mbali na mamia ya nyumba na maeneo ya vijiji yaliyochomwa moto na kundi hilo.
Mwaka uliopita, nchi za Niger, Chad, Cameroon na mwenyeji Nigeria ziliunda kikosi cha pamoja cha askari 8,700 kwa madhumuni ya kulitokomeza kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram ambalo limekuwa tishio kwa uthabiti wa eneo hilo na Afrika kwa jumla.