Kongo kuunda serikali ya mpito ikisubiri uchaguzi mkuu
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i15400-kongo_kuunda_serikali_ya_mpito_ikisubiri_uchaguzi_mkuu
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo itaunda serikali ya muda itakayowajumuisha wapinzani, ikiwa ni sehemu ya makubaliano ya kuandaa uchaguzi mpya na kutatua mgogoro wa kisiasa uliogubika nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 15, 2016 23:32 UTC
  • Kongo kuunda serikali ya mpito ikisubiri uchaguzi mkuu

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo itaunda serikali ya muda itakayowajumuisha wapinzani, ikiwa ni sehemu ya makubaliano ya kuandaa uchaguzi mpya na kutatua mgogoro wa kisiasa uliogubika nchi hiyo.

Waziri wa Sheria wa Kongo, Alexis Thambwe Mwamba ameyasema hayo baada ya waungaji mkono wa Rais Joseph Kabila na baadhi ya wapinzani kukubaliana kuhusu wakati wa kufanyika uchaguzi; suala ambalo limesababisha mjadala kwa zaidi ya mwaka mmoja na kuibua ghasia na machafuko nchini humo. Licha ya kufikiwa mapatano hayo, lakini vyama vingi vikubwa vya upinzani nchini Kongo vimesusia mazungumzo ya kitaifa yaliyoitishwa na Rais Jpseph Kabila.

Rais Kabila wa Kongo 

Vyama hivyo vinayachukulia mazungumzo hayo kama sehemu ya mpango wa Rais Kabila wa kutaka kuhalalisha kuendelea kuweko madarakani baada ya kumaliza muhula wake wa pili mwezi Disemba mwaka huu; ilhali anapasa kuondoka madarakani kwa mujibu wa katiba. Hata hivyo hadi sasa bado haijafahamika ni shakhsia wepi wa upinzani ambao watakuwa sehemu ya serikali hiyo mpya ya Kongo.

Serikali ya Kinshasa na baadhi ya vyama vya upinzani Jumatano wiki hii vilikubaliana kuwa, uchaguzi wa rais ujumuishwe na chaguzi za bunge na mabaraza ya miji, japokuwa hadi sasa hakuna tarehe maalumu iliyoainishwa kwa ajili ya kufanyika chaguzi hizo. Uchaguzi wa serikali za mitaa umepangwa kufanyika baada ya chaguzi hizo zilizotajwa.