40 wauawa Libya katika hujuma ya ndege ya Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i1546-40_wauawa_libya_katika_hujuma_ya_ndege_ya_marekani
Mashambulizi ya anga yaliyotekelezwa na ndege ya kivita ya Marekani yamesababisha mauaji ya watu zaidi ya 40 katika mji wa Sabratha, kaskazini magharibi mwa Libya.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 19, 2016 10:05 UTC
  • 40 wauawa Libya katika hujuma ya ndege ya Marekani

Mashambulizi ya anga yaliyotekelezwa na ndege ya kivita ya Marekani yamesababisha mauaji ya watu zaidi ya 40 katika mji wa Sabratha, kaskazini magharibi mwa Libya.

Hussein al-Thwadi, Meya wa mji huo amethibitisha kutokea mauaji hayo yaliyosababishwa na hujuma za ndege ya Marekani dhidi ya jengo moja ambalo lilikuwa makaazi ya raia wa kigeni, katika wilaya ya Talil. Meya huyo amesema watu 41 wameuawa na wengine 6 wamejeruhiwa katika hujuma hiyo. Amesema kuwa miongoni mwa watu waliouawa katika mashambulizi hayo ya leo asubuhi ni raia wa Tunisia na Jordan. Kwa mujibu wa Mark Cheadle, msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) tawi la Afrika, mashambulizi hayo ya anga eti yalilenga kumuangamiza Nouruddin Chouchane, kamanda mwandamizi wa kundi la kigaidi la Tunisia, ambalo linaaminika kuwa na mafungamano na kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh. Hii ni katika hali ambayo, Jumatano iliyopita Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Libya alisema kuwa, huenda hivi sasa usiwe wakati mwafaka wa kufanya operesheni za kijeshi dhidi ya magaidi wa Daesh nchini Libya. Gazeti la Ra'yul Yaum lilimnukuu Martin Kobler, mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa katika kadhia ya Libya akitoa matamshi hayo ya kutatanisha na kudai kuwa, kama hivi sasa kutaanza operesheni za kijeshi dhidi ya kundi la kigaidi la Daesh, basi kuna uwezekano suala hilo likavuruga juhudi za kuunda serikali ya umoja wa kitaifa nchini humo. Magaidi wa Daesh wanashikilia miji na vijiji kadhaa nchini Libya hususan mji wa Sirte.