Wapinzani wapambana na polisi katika mji wa Lubumbashi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i15505-wapinzani_wapambana_na_polisi_katika_mji_wa_lubumbashi
Duru za kuaminika zimetangaza habari ya kuzuka mapigano baina ya polisi na wafuasi wa chama kikuu cha upinzani huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, katika mji wa Lubumbashi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 17, 2016 10:35 UTC
  • Wapinzani wapambana na polisi katika mji wa Lubumbashi

Duru za kuaminika zimetangaza habari ya kuzuka mapigano baina ya polisi na wafuasi wa chama kikuu cha upinzani huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, katika mji wa Lubumbashi.

Vyombo vya habari vimeripoti kuwa, wafuasi wa chama kikuu cha upinzani cha UDPS cha Étienne Tshisekedi, jana Ijumaa walikabiliana na polisi katika mji wa Lubumbashi, wa kusini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, baada ya polisi kujaribu kuvunja maandamano yao.

Habari zinasema kuwa, polisi walitumia mabomu ya kutoa machozi kuwatawanya waandamanaji hao ambao walikuwa wamefunga barabara kwa kuchoma matairi ya gari. Hata hivyo, sababu za kufanyika maandamano hayo hazijatangazwa.

Maandamano ya wapinzani mjini Kinshasa, DRC

 

Duru za polisi nchini Kongo zimesema kuwa, waandamanaji hao walikuwa wanashinikiza kufanyika uchaguzi wa rais kwa muda ulioainishwa na katiba ya nchi hiyo.

Ikumbukwe kuwa, Étienne Tshisekedi, mkuu wa chama cha upinzani cha UDPS cha Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ameitisha maandamano ya nchi nzima siku ya Jumatatu ya tarehe 19 Septemba, kwa ajili ya kushinikiza kuheshimiwa katiba ya nchi hiyo.