Ubelgiji yataka ufanyike uchunguzi huru kuhusu machafuko ya Kongo DR
Serikali ya Ubelgiji imetaka ufanyike uchunguzi huru kuhusu machafuko yaliyotokea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Ubelgiji imetoa taarifa ikieleza wasiwasi mkubwa ilionao kutokana na hali inayotawala nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Mbali na kusisitiza juu ya kuanzishwa uchunguzi huru kuhusu ghasia na machafuko yaliyotokea nchini Kongo DR, serikali ya Ubelgiji imetoa wito kwa vikosi vya usalama na vya jeshi la Kongo kurejesha utulivu na amani.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Ubelgiji aidha imeeleza kupitia taarifa hiyo kuwa ufumbuzi wa mgogoro uliojitokeza utapatikana kupitia mazungumzo tu, kwa njia za amani na kwa kufuata Katiba ya nchi.
Machafuko nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo yalipamba moto kuanzia mwanzoni mwa juma lililopita baada ya maandamano ya wapinzani ya kulalamika uamuzi wa kuakhirishwa tarehe ya uchaguzi mkuu wa rais.
Zaidi ya watu 50 wameuawa na kujeruhiwa katika mapigano kati ya polisi na waandamanaji.
Ikiwa imesalia takribani miezi mitatu kabla ya kipindi cha uongozi wa Rais Joseph Kabila kumalizika, wapinzani wanamtuhumu kiongozi huyo kuwa ana mpango wa kutaka kuendelea kubaki madarakani.../