Burundi: Tuko tayari kuzungumza na Rwanda kumaliza tofauti zetu
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i1597-burundi_tuko_tayari_kuzungumza_na_rwanda_kumaliza_tofauti_zetu
Serikali ya Burundi imetangaza azma yake ya kufanya mazungumzo na Rwanda kwa lengo la kuhitimisha mivutano iliyozuka kati ya pande mbili tangu miezi kadhaa iliyopita.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 20, 2016 04:44 UTC
  • Burundi: Tuko tayari kuzungumza na Rwanda kumaliza tofauti zetu

Serikali ya Burundi imetangaza azma yake ya kufanya mazungumzo na Rwanda kwa lengo la kuhitimisha mivutano iliyozuka kati ya pande mbili tangu miezi kadhaa iliyopita.

Hayo yamedokezwa na Gaston Sindimwo, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Burundi aliyesisitiza kuwa, Bujumbura inapendelea njia pekee ya mazungumzo kwa ajili ya kuhitimisha mivutano iliyopo baina ya pande mbili. Aidha afisa huyo wa serikali ya Burundi ameitaja Rwanda kama mchochezi na msababishi wa matatizo yanayoendelea nchini kwake. Ameongeza kuwa, sasa umefika muda kwa seikali ya Kigali kuhitimisha mwenendo wake wa kiuchokozi na kuibua machafuko nchini Burundi na kusisitiza kuwa, katika fremu hiyo, mazungumzo ndiyo njia pekee mwafaka. Gaston Sindimwo amekadhibisha pia uepo wa mgogoro wa kisiasa nchini Burundi na kudai kuwa, jamii ya kimataifa inafahamu hali ya mambo kupitia kile kinachopandikizwa na Rwanda kuhusu nchi hiyo. Itafahamika kuwa, kwa mara kadhaa viongozi wa Burundi wamekuwa wakikadhibisha habari ya kuwepo machafuko nchini humo na kudai kuwa kile kinachojiri ni makabiliano baina ya polisi na kundi la watu wahuni tu. Mgogoro baina ya Kigali na Bujumbura ulishadidi baada ya wataalamu wa Umoja wa Mataifa kutoa ripoti iliyothibitisha madai ya Burundi kwamba, Rwanda imekuwa ikiwapatia Warundi mafunzo ya kijeshi kwa lengo la kuiondoa madarakani serikali ya Rais Pierre Nkurunziza, tuhuma ambazo zilipingwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda Bi. Louise Mushikiwabo.