Serikali ya Burundi yataka kufanya mazungumzo na Rwanda
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i1600-serikali_ya_burundi_yataka_kufanya_mazungumzo_na_rwanda
Serikali ya Burundi imewatolea wito viongozi wa Rwanda kufanya mazungumzo na kuhitihimisha hitilafu zilizojitokeza kati ya nchi mbili hizo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 20, 2016 09:43 UTC
  • Serikali ya Burundi yataka kufanya mazungumzo na Rwanda

Serikali ya Burundi imewatolea wito viongozi wa Rwanda kufanya mazungumzo na kuhitihimisha hitilafu zilizojitokeza kati ya nchi mbili hizo.

Gaston Sindimwe Makamu wa Kwanza wa Rais wa Burundi jana aliitaka serikali ya Rwanda kujongea kwenye meza ya mazungumzo ili kuhitimisha hitilafu kati ya nchi mbili hizo. Sindimwo amesisitiza kuwa serikali ya Rwanda inapasa kusitisha hatua zake za kusababisha ukosefu wa amani huko Burundi na kusema kuwa njia pekee ya ufumbuzi katika mazingira ya sasa ni kufanya mazungumzo. Serikali ya Burundi inamtuhuhumu Rais Paul Kagame wa Rwanda kuwa nchi yake inawatumia na kuwapa mafunzo wakimbizi wa Burundi. Kwa mujibu wa madai hayo, serikali ya Rwanda ambayo imewapokea wakimbizi wa Burundi karibu elfu 75, baada ya kuwapa mafunzo ya kijeshi, huwatumia vibaya wakimbizi hao kutekeleza mauaji ya kisiasa ya viongozi wa Burundi na kujaribu kuupindua utawala ulioko madarakani.

Rais Paul Kagame amepinga madai hayo, na wiki iliyopita alitangaza kwamba serikali yake imeamua kuwafukuza wakimbizi wa Burundi walioko Rwanda. Radiamali ya kwanza aliyoionyesha Rais wa Rwanda kwa tuhuma zilizoelekekwa kwake na serikali ya Burundi ilikuwa ni kuwafukuza huko Rwanda wakimbizi wa Burundi. Hii ni katika hali ambayo Rais Paul Kagame amemtaka mwenzake wa Burundi ajiepushe kukaririwa tena maangamizi ya kizazi na machafuko ya kikabila nchini humo. Kagame ametahadharisha kuwa iwapo mapigano kati ya wapinzani na wale wanaounga mkono kurefushwa muda wa kuweko madarakani Pierre Nkurunziza kwa kipindi kingine cha tatu hayatasitishwa; si jambo lililo mbali kutokea maangamizi ya kizazi au mauaji ya umwagaji damu huko Burundi, kama yale yaliyotokea kati ya mwezi Aprili hadi Julai mwaka 1994 huko Rwanda.

Watu wasiopungua 439 wameaga dunia kwenye mapigano tangu kufanyika uchaguzi wa Rais wa Burundi mwezi Julai mwaka jana ambao Pierre Nkurunziza aliweza kutetea kiti chake kwka muhula mwingine wa tatu. Katika kipindi hicho, raia wa Burundi karibu 230,000 walilazimika kuzihama nyumba zao na kukimbilia katika nchi jirani kama Rwanda na Tanzania kwa ajili ya hifadhi kwa kuhofia mapigano kati ya wapinzani wa serikali na vikosi vya usalama. Kuhusiana na suala hilo, Alain Guillaume Bunyoni Waziri wa Usalama wa Burundi ameihakikishia jamii ya kimataifa kuwa oparesheni ya kupokonya silaha nchini humo itaendelea na vikosi vya usalama vitaendelea kuwepo katika maeneo yaliyoathiriwa na hali ya mchafuko hadi pale amani na uthabiti utakaporejea Burundi.

Pamoja na hayo yote kupatikana makaburi tisa ya umati huko Burundi, moja likiwa limekutwa katika kambi ya kijeshi nchini humo; kunazidisha wasiwasi kuhusu kuhusika vikosi vya usalama na vile vya jeshi la Burundi katika kuwauwa raia wa nchi hiyo. Wataalamu wa Umoja wa Mataifa wametahadharisha kuwa zipo zinazoashiria hatari ya kujiri vita vya kikabila huko Burundi kati ya kabila la waliowengi la Wahutu na Watutsi walio wachache.

Mwaka uliopita Marais wa nchi za Jumuiya ya Ushirikiano wa Kieneo ya Mashariki mwa Afrika (Igad) walimteuwa Rais Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda kuwa msuluhishi kati ya wapinzani na serikali ya Burundi, hata hivyo Museveni hadi sasa jitihada zake hazijazaa matunda. Weledi wa mambo wanaamini kuwa Museveni ambaye kwa miongo mitatu mtawalia amekuwa akishikilia hatamu za uongozi huko Uganda, si chaguo sahili la kuweza kumshawishi Nkurunziza aondoke madarakani.

Baadhi ya pande zimempendekeza Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini kuchukua nafasi ya Museveni ya upatanishi katika mgogoro wa Burundi. Wakati huo huo vyama vya upinzani nchini Afrika Kusini vimemtaka Zuma ajiuzulu kutokana na ufisadi wa fedha za umma na tuhuma nyinginezo zinazomkabili. Katika mazingira hayo Rais John Pombe Magufuli wa Tanzania huenda akawa chaguo linalofuata. Inaonakena kuwa safari ya hivi karibuni ya Augustine Mahiga Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa wa Tanzania ilihusiana na suala hilo. Ombi la serikali ya Burundi la kufanya mazungumzo na jirani yake Rwanda huenda ni natija ya ziara hiyo yenye lengo la kuipatia ufumbuzi mivutano ya kisiasa na kuhuisha uhusiano wa nchi mbili hizo jirani ulioingia dosari.