Wanajeshi wanane wa Nigeria wauawa na wanamgambo wa Boko Haram
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i16126-wanajeshi_wanane_wa_nigeria_wauawa_na_wanamgambo_wa_boko_haram
Jeshi la Nigeria limetangaza kuwa, wanajeshi wake wanane wameuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa kufuatia shambulio la wanamgambo wa Boko Haram kaskazini mashariki mwa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 26, 2016 10:50 UTC
  • Wanajeshi wanane wa Nigeria wauawa na wanamgambo wa Boko Haram

Jeshi la Nigeria limetangaza kuwa, wanajeshi wake wanane wameuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa kufuatia shambulio la wanamgambo wa Boko Haram kaskazini mashariki mwa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.

Taarifa ya jeshi la Nigeria imeeleza kuwa, shambulio lililofanywa na kundi la kigaidi la Boko Haram yapata kilomita 110 kaskazini mashariki mwa mji wa Maiduguri katika jimbo la Borno limepelekea kwa uchache wanajeshi wanane wa nchi hiyo kuuawa na wengine 17 kujeruhiwa.

Kuuawa wanajeshi hao wa Nigeria kunajiri masaa kadhaa tu baada ya jeshi la nchi hiyo kuatangaza kuwa, limewaua wanachama wasiopungua 22 wa kundi la Boko Haram.

Wanajeshi wa Nigeria wakiwa katika moja ya maeneo yanayokabiliwa na mashambulio ya Boko Haram

Msemaji wa jeshi la Nigeria amenukuliwa akisema kuwa, jeshi hilo linaendelea na opereseheni zake za kupambana na kundi la kigaidi la Boko Haram, na kuongeza kuwa, wanachama 22 wa kundi hilo wameuawa katika opereseheni ya karibuni kabisa.

Kanali Sani Kukasheka Usman aaliwaambia wanahabari hapo jana kwamba, wanamgambo hao waliuawa kwenye  jimbo la Borno katika mapigano na jeshi la Nigeria.

Watu wasiopungua 20 elfu wameripotiwa kuuawa na milioni mbili na laki sita wengine wamepoteza makazi yao tangu kundi hilo la kitakfiri lilipoanzisha mashambulizi yake nchini Nigeria mwaka 2009.

Kundi hilo limepanua mashambulizi yake hadi katika nchi jirani za Cameroon, Niger na Chad.

Hivi sasa kumeundwa jeshi la nchi nne za Nigeria, Niger, Chad na Cameroon kwa ajili ya kupambana na genge hilo hasa kwenye eneo la Ziwa Chad.