Uchaguzi mkuu wa Somalia waakhirishwa tena
Serikali ya Somalia imetangaza kuwa uchaguzi mkuu wa nchi hiyo uliokuwa umepangwa kuanza kufanyika mwezi ujao wa Oktoba umeakhirishwa na kusogezwa mbele hadi mwezi Novemba kutokana na matatizo ya kiusalama na kiidara.
Maafisa wa Tume ya Uchaguzi ya Somalia wameeleza kupitia taarifa kwamba uchaguzi wa Bunge utafanyika kati ya tarehe 23 Oktoba hadi tarehe 10 Novemba, na ule wa Rais umepangwa uwe umeshafanyika hadi ifikapo tarehe 30 Novemba.
Taarifa hiyo ya Tume ya Uchaguzi imefafanua kuwa licha ya kazi kubwa iliyofanywa kwa ajili ya maandalizi ya uchaguzi kuna baadhi ya mambo bado hayajaweza kukamilishwa kwa wakati uliopangwa; na baadhi ya malengo pia hayajaweza kufikiwa kutokana na sababu za kisiasa, matatizo ya kiusalama na masuala yanayohusiana na bajeti ya uchaguzi wenyewe.
Tarehe za uchaguzi mkuu wa Somalia zimeakhirishwa mara kadhaa hadi sasa katika hali ambayo Umoja wa Afrika na Jumuiya ya IGAD zilitoa wito hivi karibuni wa kuvitaka vyama vyote vya siasa pamoja na wananchi wa Somalia kushiriki kikamilifu katika mchakato wa uchaguzi wa nchi yao na kufanya juhudi kuhakikisha uchaguzi huo unafanyika katika anga ya kidemokrasia. Mbali na viongozi wa nchi za Afrika kueleza jinsi walivyosikitishwa na kuakhirishwa mara kadhaa utekelezaji wa ratiba za uchaguzi mkuu wa Somalia wamevitaka vyama na wadau wote wanaohusika katika mchakato wa kisiasa wa nchi hiyo kuhakikisha ratiba iliyopangwa kuhusiana na wakati wa kufanyika uchaguzi huo inaheshimiwa na kutoifanyia mabadiliko mengine mapya ratiba hiyo.../