Kushadidi ghasia katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo
Kuendelea maandamano dhidi ya serikali katika mji mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Kinshasa kumepelekea watu zaidi kuuawa.
Katika hali ambayo Lambert Mende Omalanga Waziri wa Habari na msemaji wa serikali ya DRC ametangaza kuwa idadi ya wahanga wa machafuko hayo mjini Kinshasa ni watu 32, wapinzani wanasema kuwa, waliouawa katika ghasia hizo ni watu 100. Wakati huo huo kwa akali watu 46 wamepoteza maisha huko Kasai na Kananga katika vurugu baina ya polisi na raia wanaolalamikia kuongezwa utawala wa Rais Joseph Kabila.
Kupanuka wigo wa malalamiko kutoka mji mkuu Kinshasa na kuenea katika majimbo mengine ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ni ishara tosha ya kuvurugika hali ya usalama na hii inaonyesha kwamba, kama hali hiyo itaendelea, basi serikali na vikosi vya usalama vitashindwa kudhibiti hali ya mambo. Rais Kabila ambaye anawatuhumu wapinzani kwamba, wameanzisha uasi wa umwagaji damu alielekea Vatican na amekutana na kufanya mazungumzo na Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani Papa Francis.
Hata kama kile walichozungumza Rais Kabila na Papa Francis bado hakijajulikana, lakini kile ambacho kiko wazi ni kwamba, matukio ya umwagaji damu huko DRC ndio iliyokuwa ajenda kuu ya mazungumzo yao. Weledi wa mambo wanaamini kuwa, katika hali ambayo, waandamanaji na wafuasi wa muungano wa kisiasa wa wapinzani wanataka Rais Joseph Kabila aachie ngazi, kiongozi huyo na serikali yake wanaendelelea kuyakandamiza maandamano mjini Kinshasa na kutumia mkono wa chuma kuwasambaratisha waandamanaji.
Kikosi cha Gadi ya Rais ambacho kiko chini ya Rais na kinapokea amri moja kwa moja kutoka kwa Rais Kabila kimekuwa kikiwakandamiza waandamanaji katika mitaa ya mji wa Kinshasa. Bruno Tshibala, kiongozi wa muungano wa upinzani amesema kuwa, kupelekwa kikosi cha Gadi ya Rais katika mitaa ya Kinshasa kunakinzana na demokrasia.
Akthari ya wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanaamini kuwa, kung'ang'ania Rais Kabila kuzima sauti ya wapinzani kunaonyesha azma aliyo nayo ya kuendelea kubakia madarakani. Muungano wa wapinzani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo umefadhilisha kumiminika katika mitaa na barabara za mji mkuu Kinshasa na miji mingine badala ya kukaa katika meza moja ya mazungumzo na serikali ili sambamba na kumuonyesha nguvu yao Rais Kabila uzuie pia kuongezwa muda wa rais huyo kuendelea kubakia madarakani. Hadi sasa Kamisheni ya Uchaguzi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo haijaainisha tarehe mpya ya kufanyika uchaguzi nchini humo; lakini kwa mujibu wa hukumu ya Mahakama Kuu Rais Kabila anapaswa kubakia madarakani hadi pale uchaguzi mwingine utakapofanyika.
Kwa muktadha huo, Rais Kabila ana uhakika wa kubakia madarakani mpaka utakapofanyika uchaguzi mwingine, isipokuwa kikwazo pekee kwa sasa ni maandamano dhidi ya serikali. Ni kwa kuzingatia uhakika huo, ndio maana licha ya kuweko ukosoaji mkubwa wa asasi za kutetea haki za binadamu serikali ya Rais Kabila ikaendelea na ukandamizaji dhidi ya waandamanaji na wapinzani wa serikali. Endapo serikali ya DRC itakabiliwa na mashinikizo ya kisiasa ya asasi za kimataifa kama Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika, Umoja wa Ulaya na Jumuiya ya Francophone na kulazimika kuitisha uchaguzi, basi hiyo itakuwa ni natija ya muungano unaoshuhudiwa mara hii baina ya vyama vya upinzani nchini humo.
Katika uchaguzi wa mwaka 2011 kulishuhudiwa mgawanyiko baina ya wapinzani suala lililopelekea mrengo wa upinzani kushindwa kusimamaisha mgombea mmoja kwa ajili ya kuchuana na Rais Kabila. Umoja na mshikamano uliopo hivi sasa baina ya wapinzani ambao ni ubunifu wa Étienne Tshisekedi mwanasiasa mkongwe wa nchi hiyo ni karata yao ya turufu ya kushindana na Rais Kabila katika uchaguzi ujao.