Wanajeshi 17 wa Somalia wauawa katika mapigano baina ya maeneo yanayojitawala
Wanajeshi wasiopungua 17 wameuawa usiku wa kuamkia leo katika mapigano baina ya vikosi vya maeneo mawili yenye mamkala ya ndani kaskazini mwa Somalia.
Maafisa wa usalama wanasema wanajeshi wa Puntland na Galmudug wamepigana kutokana na mzozo wa mpaka na uhasma wa kisiasa.
Maafisa wa Puntland wanasema wamewaua magaidi katika hujuma ya anga lakini wakuu wa Galmudug wanasema wanajeshi wa eneo hilo ndio waliolengwa na kuuawa.
Abdu Hussein, Naibu Gavana wa Galkayo, mji mkuu wa eneo la Galmudug amesema madai ya Puntland ni propaganda kwani wanajeshi 17 wa Galmudug wameuawa na magari mawili ya kijeshi kuharibiwa katika hujuma hiyo ya anga.

Hata hivyo Kanali Abdullahi Nur wa Puntland amesisitiza kuwa vikosi vya eneo hilo vimewalenga magaidi.
Eneo la Puntland liko kaskazini mashariki mwa Somalia na mwaka 1998 lilijitangazia mamlaka ya ndani lakini lingali chini ya usimamizi wa Shirikisho la Jamhuri ya Somalia.
Eneo la Galmudug nalo lilijitangazia mamlaka ya ndani mwaka 2013 chini ya uongozi wa Mohammad Warsame Ali maarufu kama Kiimiko. Kumekuwepo na mzozo wa muda mrefu baina ya maeneo hayo mawili.