Marekani yadai kufanya makosa katika kuwaua askari 22 wa Somalia
Askari wa Marekani wametuhumiwa kuhusika na mauaji ya askari 22 wa Somalia katika kile kinachodaiwa kuwa ni makosa yaliyofanyika katika urushaji makombora ya ndege kaskazini mwa nchi hiyo ya Kiafrika.
Jana Jumatano, Osman Issa, Waziri wa Usalama wa eneo lililojitangazia mamlaka ya ndani la Galmudug alisema kuwa askari hao waliuawa katika shambulio hilo la anga na kuongeza kuwa shambulio hilo lilitekelezwa na Wamarekani baada ya kuombwa na eneo jingine jirani la Puntland ambalo pia lilijitangazia mamlaka ya ndani miaka kadhaa iliyopita, kwa kisingizio kuwa walikuwa ni magaidi wa as-Shabaab. Kaptain Jeff Davis msemaji wa Pentagon alidai kwamba askari wa Marekani walilazimika kufanya mashambulio hayo ya anga katika kile alichotaja kuwa ni kujitetea dhidi ya wanamgambo wa as-Shabaab baada ya kushambuliwa na askari wa Somalia waliokuwa wakitekeleza operesheni dhidi ya kituo chao cha kutengenezea mabomu.
Amesema magaidi 9 wa As-Shabaab waliuawa katika shambulio hilo na kutilia shaka ripoti zinazosema kuwa askari 22 wa Somalia pia waliuawa katika shambulia hilo la anga. Polisi ya Puntland imesema kuwa zaidi ya magaidi 12 wa Puntland waliuawa katika shambulio hilo. Kwa upande wao as-Shabaab wanadai kwamba hakuna mwanachama wao hata mmoja aliyeuawa katika shambulio hilo kwa sababu hawakuwa na wapiganaji katika eneo hilo wakati ya kufanyika shambulio hilo.
Somalia imekuwani uwanja wa mapigano kati ya jeshi na serikali na magaidi wa as-Shabaab wanaotaka kuipindua tokea mwaka 2006. Mwaka 2011 magaidi hao walifukuzwa na kusogezwa nyuma kutoka mji mkuu wa nchi hiyo Mogadishu na askari jeshi wa serikali wanaosaidiwa na kikosi cha Umoja wa Afrika AMISOM ambacho kimsingi kinaundwa na askari kutoka nchi za Ethiopia, Uganda, Burundi, Djibouti na Kenya.