Mazungumzo ya kitaifa yaanza tena Congo DR
Mpatanishi katika mazungumzo ya kitaifa huko katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ametangaza kuwa, mazungumzo ya kitaifa ya nchi hiyo yalianza Ijumaa ya jana katika mji mkuu wa nchi hiyo, Kinshasa.
Edem Kodjo Waziri Mkuu wa zamani wa Togo na msimamuzi wa mazungumzo ya kitaifa ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo amesema kuwa, pande mbalimbali zinashiriki katika mazungumzi hayo ya kitaifa.
Amebainisha kuwa, pande husika zimeafikiana kuhusiana na rasimu aliyokuwa ameipendekeza kuhusiana na utatuzi wa mgogoro wa nchi hiyo. Mazungumzo hayo yameanza baada ya mji mkuu Kinshasa kushuhudia mauaji makubwa tarehe 19 na 20 za mwezi uliopita wa Septemba.
Mauaji hayo yalitokea baada ya askari usalama kukabiliana na waandamanaji waliokuwa wakipinga kile walichokiitaja kuwa, njama za serikali ya Rais Joseph Kabila za kutaka kubakia madarakani.
Serikali ya Kinshasa inasema ni watu 32 tu ndio waliopoteza maisha katika vurugu baina ya wapinzani na askari wa serikali huku mrengo wa upinzani na mashirika ya kutetea haki za binadamu yakisema kuwa, zaidi ya watu 100 waliuawa katika vurugu hizo.
Rais Kabila mwenye umri wa miaka 45 ambaye yupo madarakani tangu kuuliwa baba yake mwaka 2001, anakabiliwa na mashinikizo ya ndani na ya madola makubwa yanayomtaka aachie madaraka na kuitisha uchaguzi wa rais baada ya muhula wake kumalizika mwezi Novemba mwaka huu.