Wapinzani DRC wakutana Kinshasa kulalamikia kuakhirisha uchaguzi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i16735-wapinzani_drc_wakutana_kinshasa_kulalamikia_kuakhirisha_uchaguzi
Wapinzani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo jana walifanya mkutano katika mji mkuu wa nchi hiyo Kinshasa na kulalamikia hatua ya Tume ya Uchaguzi ya kuakhirisha zoezi la uchaguzi mkuu uliokuwa ufanyike mwezi ujao wa Novemba.
(last modified 2026-02-25T03:34:48+00:00 )
Oct 05, 2016 04:37 UTC
  • Wapinzani DRC wakutana Kinshasa kulalamikia kuakhirisha uchaguzi

Wapinzani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo jana walifanya mkutano katika mji mkuu wa nchi hiyo Kinshasa na kulalamikia hatua ya Tume ya Uchaguzi ya kuakhirisha zoezi la uchaguzi mkuu uliokuwa ufanyike mwezi ujao wa Novemba.

Wapinzani hao wametoa mapendekezo yao ya kufanyika mazungumzo ya kitaifa sambamba na kufanyika haraka iwezekanavyo uchaguzi wa nchi hiyo. Mapendekezo hayo yanatolewa siku chache tu baada ya mazungumzo ya kitaifa ya nchi hiyo kukabiliwa na mkwamo.

Aidha wapinzani hao wamekutana siku chache tu baada ya Tume ya Uchaguzi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kutangaza kuwa, uchaguzi ujao wa Rais nchini humo utafanyika mwaka 2018.

Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo

Tangazo hilo la Tume ya Uchaguzi linamaanisha kwamba, Rais Kabila ambaye muhula wake wa uongozi unamalizika Disemba mwaka huu ataendelea kubakia madarakani. Mahakama Kuu ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ilitangaza kuwa iwapo itashindikana kuanda uchaguzi wa rais katika wakati ulioainishwa basi Rais Kabila anaweza kubakia madarakani hadi wakati wa kufanyika uchaguzi mkuu. 

Katika upande mwingine wapinzani wa nchi hiyo wameendelea kumtuhumu Edem Kodjo mpatanishi wa Umoja wa Afrika katika mgogoro wa Jamhuri ya Kidemorasia ya Congo kwamba, anaipendelea serikali na wametaka ajiuzulu nafasi yake hiyo.

Rais Kabila alishika hatamu za kuiongoza Kongo mwaka 2001 baada ya kuuawa baba yake, Laurent Kabila, na kisha akashinda uchaguzi wa rais uliofanyika mwaka 2006. Kwa mujibu  wa katiba ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Rais Joseph Kabila haruhusiwi kugombea tena kiti hicho baada ya kuhudumu kwa vipindi viwili vya miaka mitano mitano.