Rais Kabila: Uchaguzi utafanyika mwaka 2018
Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo amesisitiza kuwa uchaguzi nchini humo utafanyika mwaka 2018.
Rais Joseph Kabila alisema katika mkutano na waandishi wa habari hapo jana kuwa raia wa Kongo zaidi ya milioni kumi watapoteza fursa ya kupiga kura iwapo uchaguzi hautaakhirishwa. Wakati huo huo Corneille Nangaa Mkuu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo pia amesema kuwa uchaguzi mkuu utafanyika nchini mwezi Disemba mwaka 2018.
Hii ni katika hali ambayo Jumuiya za Kutetea Haki za Binadamu zimeiomba serikali ya Kongo itangaze kwa wakati ratiba za kufanyika uchaguzi huo na ichukue hatua za lazima kufanikisha suala hilo. Weledi wa masuala ya kisiasa wanaamini kuwa kitendo cha serikali ya Kinshasa cha kutoainisha tarehe rasmi ya kufanyika uchaguzi ni kinyume na sheria za haki za ndani ya nchi hiyo na kimataifa. Hatua hiyo ya serikali ya Kongo imesababisha maandamano dhidi ya serikali na kuzua makabiliano makali kati ya waandamanaji na polisi katika mitaa ya mji mkuu Kinshasa.