Chama cha Kiislamu Morocco chapata ushindi viti Bunge
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i16978-chama_cha_kiislamu_morocco_chapata_ushindi_viti_bunge
Chama cha Kiislamu cha Uadilifu na Maendeleo (PJD), ambacho kwa miaka mitano kimeongoza serikali ya mseto Morocco, kinatazamiwa kupata ushindi katika uchaguzi wa Bunge, matokeo ya awali yameonyesha.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 08, 2016 04:34 UTC
  • Chama cha Kiislamu Morocco chapata ushindi viti Bunge

Chama cha Kiislamu cha Uadilifu na Maendeleo (PJD), ambacho kwa miaka mitano kimeongoza serikali ya mseto Morocco, kinatazamiwa kupata ushindi katika uchaguzi wa Bunge, matokeo ya awali yameonyesha.

Wagombea wa PJD wameshinda viti 99 vya Bunge katika uchaguzi uliofanyika Ijumaa huku chama kiliberali cha PAM kikipata viti 80. Asilimia 90 ya kura zimeshahesabiwa.

Chama cha Istiqlal (Uhuru) ambacho kiliongozi mapambano ya kupigania uhuru wa nchi hiyo kutoka mkoloni Mfaransa ni cha tatu kwa kupata viti 31 kikifuatiwa na vyama vingine kadhaa vidogo.

Ni asilimia 43 tu ya wapiga kura, yaani watu milioni sita na laki saba, waliojitokeza kupiga kura katika uchaguzi huo ambao umegubikwa na madai ya wizi wa kura.

Alama ya kidole baada ya upigaji kura

Chama cha Kiislamu cha PJD kiliingia madarakani nchini Morocco mwaka 2011 baada ya miezi kadhaa ya maandamano yaliyofanyika kufuatia wimbi la mwamko wa Kiislamu katika nchi za Kiarabu. Chama hicho cha PJD kinadaiwa kuwa na uhusiano wa karibu na mfalme wa nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.