Kiongozi wa upinzani atiwa nguvuni Kongo DR
Kiongozi mmoja wa upinzani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ametiwa nguvuni kwa madai ya kuhusika na machafuko yaliyotokana na maandamano ya kupinga serikali yaliyofanyika mwezi uliopita ambapo watu zaidi ya 50 waliuawa.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na chama chake, Bruno Tshibala, Naibu Katibu Mkuu na msemaji wa chama kikuu cha upinzani nchini Kongo DR cha Muungano kwa ajili ya Demokrasia na Maendeleo ya Kijamii (UDPS) alikamatwa usiku wa kuamkia jana katika uwanja wa ndege wa mji mkuu wa nchi hiyo Kinshasa wakati akijiandaa kupanda ndege kuelekea Brussels, Ubelgiji.
Kutiwa nguvuni kiongozi huyo kumezidsha wasiwasi wa kushuhudiwa maandamano zaidi ya upinzani endapo hatoachiwa huru.
Msemaji wa serikali Lambert Mende amethibitisha taarifa za kutiwa nguvuni Tshibala na kueleza kwamba kiongozi huyo wa upinzani atahojiwa na ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa serikali kuhusiana na nafasi yake katika maandamano ya upinzani ikiwemo vifo vya afisa mmoja wa polisi aliyechomwa moto akiwa hai pamoja na msichana mmoja.
"Yeye ni miongoni mwa watu walioandaa maandamano ya Septemba 19 na 20. Tshibala alisaini taarifa ambapo aliwapongeza waandamanaji", amesema Mende.
Mwanasheria Mkuu wa serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo amesema atatoa adhabu kwa watu walioandaa maandamano ambayo yalikuwa ni ya kulalamikia kile kinachodaiwa kuwa ni hatua ya Rais Joseph Kabila ya kuhakikisha anaendelea kubakia madarakani baada ya kipindi chake cha pili na cha mwisho cha uongozi kumalizika ifikapo mwezi Desemba mwaka huu.
Wakati huohuo Katibu Mkuu wa chama cha UDPS Jean Marc Kabund ameahidi kuwa maandamano yataanza tena kesho Jumatano endapo Bruno Tshibala hatoachiwa huru.../